Maureen Mwanawasa alikuwa mke wa rais wa Zambia kuanzia 2002 hadi 2008. / Picha: TRT Afrika

Na Brian Okoth

Mke wa Rais wa zamani wa Zambia Maureen Kakubo Mwanawasa amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 61.

Mwanawasa alifariki katika Kituo cha Matibabu cha Maina Soko katika mji mkuu Lusaka siku ya Jumanne.

Mke huyo wa zamani wa rais alifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Alikuwa mke wa Rais wa tatu wa Zambia Levy Mwanawasa, ambaye alihudumu kuanzia 2002 hadi kifo chake mwaka 2008.

'Mshtuko mkubwa na huzuni'

Rais Hakainde Hichilema alisema katika taarifa yake Jumanne kwamba kifo cha Maureen Mwanawasa kilimwacha katika "mshtuko na huzuni kubwa."

Rais Hichilema aliongeza katika taarifa yake: "Tunatoa wito kwa nchi kuungana tunapoungana na familia yake na taifa katika maombi."

Kwa Wazambia wengi, mke wa rais wa zamani alikuwa kinara wa wema, huruma, na kujitolea kwa taifa la Zambia.

Maureen Mwanawasa alizaliwa Aprili 28, 1963 huko Kabwe, mji wa Jimbo la Kati la Zambia.

Mwanasheria kwa taaluma

Alisomea shahada yake ya kwanza ya sheria katika Chuo Kikuu cha Zambia, na baadaye shahada yake ya uzamili katika usimamizi wa biashara ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Edith Cowan nchini Australia.

Aliolewa na Rais wa zamani Levy Mwanawasa, ambaye pia kitaaluma alikuwa mwanasheria, mwishoni mwa miaka ya 1980.

Walijaaliwa watoto wanne pamoja - mabinti watatu na mtoto mmoja wa kiume.

Maureen Mwanawasa alikuwa mwanachama mwanzilishi na rais wa zamani wa Shirika la Wake wa Marais wa Afrika dhidi ya VVU/UKIMWI, ambalo kwa sasa linajulikana kama Shirika la Wanawake wa Marais wa Afrika kwa Maendeleo.

Athari kubwa

Alijitolea maisha yake kutetea maendeleo ya kijamii na haki ya kijamii, na pia kuangazia maswala ya afya ya umma ulimwenguni.

Wakati wa uongozi wake kama rais wa shirika la wake wa marais wa Afrika, aliagiza matibabu ya kwanza ya kurefusha maisha ya watoto barani Afrika na kuhamasisha mataifa ya Afrika kutambua ukweli wa VVU/UKIMWI.

Kupitia Mpango wake wa Jumuiya ya Maureen Mwanawasa, mke wa rais wa zamani alitoa ufadhili wa masomo ya shule za sekondari na vyuo kwa wanafunzi kadhaa.

Athari zake kubwa kwa ubinadamu zilimfanya atambuliwe kimataifa na mashirika kadhaa.

Azma ya kisiasa

Kama vile mumewe, Mwanawasa alikuwa na ndoto ya kisiasa ndani yake.

Mnamo 2016, aligombea nafasi ya Meya wa Lusaka.

Katika kampeni yake, aliahidi kushughulikia uhaba wa maji, matatizo ya ukusanyaji wa takataka, na changamoto za usafi wa jiji.

Mwanawasa alishika nafasi ya pili, nyuma ya Wilson Kalumba wa Patriotic Front katika uchaguzi uliofanyika Agosti mwaka huo.

TRT Afrika