Huku vita ikiendelea nchini Sudan kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha Rapid Support Forces, RSF, tangu tarehe 15 Aprili mwaka huu, kuna changamoto ya wakimbizi kuzingatia.
Halime Issakh Oumar ni miongoni mwa wakimbizi waliovuka kutoka Sudan hadi Chad na kupokelewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR.
"Hakuna usalama, tulikimbia kutoka Sudan hadi Chad, tunataka kuwa salama, hakuna usalama nchini Sudan, tulikuja bila chochote," anasema.
Video zilizotolewa na UNHCR zinaonyesha wananchi wa Sudan wazee kwa vijana waliolazimika kuondoka nchini kwenda kutafuta hifadhi katika nchi jirani ya Chad. Wanawake wengine walivuka na watoto waaliokuwa wamezaliwa tu, wengine na watoto wadogo sana.
"Baadhi yetu ni wagonjwa na tunahitaji matibabu, hatuwezi kurudi nyuma, kwa sababu si salama," anasema Idriss Yaya Abddekerim, mkimbizi mwingine.
Kulingana na takwimu za UNHCR Mashariki ya Chad tayari inawahifadhi takriban wakimbizi 400,000 kutoka Sudan. Uingiaji mpya wa wakimbizi unaongeza matatizo.
"Tangu kuanza kwa mapigano, wakimbizi wasiopungua 20,000 wamekimbia kuvuka mpaka na kuingia Chad," UNHCR imesema katika taarifa.
"Hadi sasa, harakati muhimu zaidi za watu kuvuka mpaka zimekuwa ni watu wanaokimbilia Chad, na wakimbizi wa Sudan Kusini wanaorudi Sudan Kusini," inaongeza.
"Tumesajili karibu wananchi wa Sudan Kusini 4000 wakivuka mpaka kutoka Sudan," ofisi ya UNHCR nchini Sudan Kusini ilisema Jumanne. Wengi zaidi wanatarajiwa huku mzozo ukiendelea.
Wakimbizi wa Sudan Kusini waliwakilisha idadi kubwa zaidi ya wakimbizi waliohifadhiwa na Sudan, wakiwa takriban 800,000. Walikimbia ukosefu wa utulivu nchini mwao ulioanza mwaka 2013 na sasa wengi wanalazimika kurejea.
Dkt. Edgar Githua mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa anasema hata nchi zisizo na mipaka ya moja kwa moja na Sudan zitabeba mzigo mkubwa wa wakimbizi.
"Kenya na Uganda ziwe tayari kurithi idadi kubwa ya wakimbizi hawa kutoka Sudan hata kama hazipakani na Sudan," Githua anaiambia TRT Afrika, " bila shaka hiyo italeta mzozo wa kibinadamu kwetu. Na kutokana na mzozo wa wakimbizi huenda tukapata tatizo la kuenea kwa silaha ndogo ndogo,” Githua aongezea.
"Kenya na Uganda zikuwe tayari kurithi idadi kubwa ya wakimbizi hawa kutoka Sudan hata kama hazipakani na Sudan,"
Sudan imekuwa mwenyeji mkubwa wa wakimbizi, ikiwa na takriban watu milioni moja na laki moja, kati ya idadi kubwa ya wakimbizi barani Afrika. Kando na wananchi wa Sudan Kusini ambao wanaunda idadi kubwa zaidi ya wakimbizi, takriban wakimbizi 126,000 wa Eritrea wamehifadhiwa na Sudan.
Nchi hiyo pia ilitoa makazi kwa raia wa Ethiopia zaidi ya 58,000 ambao walikimbilia Sudan kati ya mwaka 2020 na 2022. Walikimbia kutoka Ethiopia wakati mzozo kati ya serikali ya Ethiopia na vikosi vya Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF, ulipotokea.