Malaria imekuwa ni tatizo la kiafya linalopewa kipaumbele katika kanda ya Afrika katika miongo kadhaa iliyopita. Inabakia kuwa sababu kuu ya magonjwa na vifo, hasa kwa watoto wadogo na kina mama wajawazito.
Lakini sasa kuna nchi zinazojitahidi kulitokomeza janga hilo.
Misri imetangazwa kuwa huru na malaria ikiwa na maana kwamba, ili nchi iwe huru na malaria ni lazima iwe imepita miaka mitatu bila kuwepo kwa mgonjwa wa malaria ndani ya nchi.
Pia uamuzi huu hufikiwa baada ya WHO kuhakikisha kwamba nchi husika imeweka mfumo unaofanya kazi kikamilifu wa ufuatiliaji na mwitikio ambao unaweza kuzuia maambukizi mapya ya malaria.
Kuna nchi nyengine pia ambazo zimeorodheshwa na WHO kwa kutokomeza malaria, ambazo ni Algeria, Cabo Verde, Mauritius na Morocco.
Lakini pia, kuna nchi nyengine ambazo hazijawahi kuwa na malaria au malaria ilitoweka bila hata kufanyika kwa juhudi zozote maalumu. Hizi ni pamoja na Lesotho, Seychelles, Libya na Tunisia.
Licha ya hatua zilizopigwa na baadhi ya nchi, lakini malaria bado inabaki kuwa changamoto kubwa barani.
Nchi 20 kati ya zilizoathiriwa zaidi - ambazo zinachangia zaidi ya 85% ya maambukizi na vifo kutokana na Malaria - ziko katika bara Afrika.
Hii inachangiwa na changamoto kadhaa kama vile hali ya hewa, migogoro ya kibinadamu, vikwazo vya rasilimali, vitisho vya kibayolojia na ukosefu wa usawa.
Sasa kuna chanjo za malaria ambazo zimeanza kusambazwa katika nchi kadhaa barani ambazo zitatolewa katika ratiba za kawaida za chanjo ya watoto.
Huku wataalamu wa afya wakizidi kuelezea umuhimu wa kulala ndani ya vyandarua vilivyowekwa dawa, pia wanasisitiza kutumia dawa za kuua mbu na kupata matibabu haraka iwezekanavyo pindi mtu anapopata malaria.