Ripoti zinasema jeshi limelipua mabomu ya angani huku RSF wakijibu kwa Makombora ya kudungua ndege : Picha Kumbukumbu za AFP / Photo: AFP Archive

Mapigano makali yalizuka katika miji mitatu mikubwa nchini Sudan baada ya muda uliokubaliwa wa saa 72 wa kusitisha vita kumalizika.

Muda mfupi kabla ya saa kumi na mbili jioni (saa za Sudan) milio ya risasi ilisikika katika miji ya Khartoum, Bahri na Omdurman.

Walioshuhudia wanasema kuwa jeshi lilishambulia kwa mabomu ya angani mji wa Bahri huku wapiganaji wa RSF wakijibu kwa makombora ya kudingua ndege.

Shirika la Reuters limeripoti kuwa mapigano yalitokea katika kambi kuu ya jeshi mjini Dalanj, kusini mwa Kordofan, inayohusishwa na Abdel Aziz Al Hilu, mmoja wa viongozi wa SPLM-N, kundi la waasi lisilohusishwa na upande wowote wa majeshi wanaozozana.

Upande wa jeshi la serikali umemlaumu Al-Hilu na wapiganaji wake kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha vita na kusababisha uharibifu mkubwa.

Hata hivyo kumekuwa na ripoti kadhaa kuwa pande zote mbili zimekuwa zinakiuka baadhi ya makubaliano katika mkataba huo wa kusitisha vita.

Makabiliano kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha dharura cha RSF yalianza katika mji mkuu Khartoum na kisha kusambaa Magharibi mwa Darfur kwa zaidi ya miezi miwili, na kusababaisha zaidi ya watu milioni mbili kukimbia makwao.

Makubaliano hayo ya kusitisha vita ni katika juhudi nyingi za kudhibiti mapigano zinazoongozwa kwa ushirikiano wa Saudi Arabia na Marekani.

Marekani imetishia kusitisha mazungumzo hayo yanayoendelea mjini Jeddah iwapo pande husika hazitaheshimu makubaliano ya kusitisha vita.

TRT Afrika
Reuters