Mei 8, 1945, jeshi la Ufaransa chini ya kamanda wake, liliwaua raia 45,000 wa Algeria  / Photo: AP / Photo: AP Archive

Miaka 75 baadaye, bado mauaji ya halaiki, ya watu 45,000 raia wa Algeria yaliyofanywa na wanajeshi wa Ufaransa yanakumbukwa na wenyeji.

Jumanne, Mei 8, 1945 ilikuwa siku ambayo dunia nzima iliadhimisha kuporomoka kwa utawala wa kijerumani uliotazamiwa kuwa wa kikatili.

Wanajeshi wa Algeria walikuwa miongoni mwa kikosi waliopigana kum'ngoa Adolf Hitler, kiongozi wa ki imla wa Ujerumani aliye wasababishia wengi maafa duniani.

Hata hivyo, wakati dunia ikisherehekea ushindi dhidi ya Hitler, anayeaminiwa kuwaua zaidi ya Wayahudi milioni sita wa kizungu, na wengine milioni tano wafungwa wa kivita, kulikuwa na mauaji ya kikatili katika miji ya Algeria - Wanajeshi wa Ufaransa walikuwa wakiwaua kiholela raia wa nchi hiyo waliokuwa wakiandamana kupinga utawala wa kikoloni.

Wanahistoria wa kifaransa wanadai idadi hiyo ni 15,000 na sio 45,000 kama ilivyo nakiliwa katika sehemu nyingi. Hata hivyo takwimu rasmi zinaonesha kuwa idadi hiyo ilikuwa 45,000.

Jeshi hilo la Ufaransa lilikuwa linajaribu kuzima maandamano ya raia ya kupigania uhuru.

Maandamano hayo yalifanyika zaidi katika miji ya kaskazini mashariki ya Sétif na Guelma, ambako kuliripotiwa mauaji mengi zaidi.

Maandamano makubwa na umwagikaji damu

Wiki moja kabla ya hapo, Wafaransa waliweza kuvunja maandamano mengine nchini Algeria. Hata hivyo maandamano yaliyofuata ya Mei 8, yalikuwa makubwa zaidi na kusambaa sehemu nyingi na kuishia kwa mauaji mabaya ambapo watu walirushwa kutoka milimani, waandamanji wakauawa kwa maelfu, na idadi kubwa zaidi kujeruhiwa.

Mwana historia Redouane Aïnad Tabet aliandika kuwa wananchi wa Algeria walipigwa na butwaa kutokana na kilichotokea na kuwa viongozi wao wa kisiasa walikumbwa na kiwewe.

'Mauaji ya Baba mdogo yalituathiri'

Hadda Hazem, mhariri wa jarida la kila siku la Al-Fadjr, alimpoteza baba yake mdogo katika mauaji hayo ya mwaka wa 1945.

Ameambia TRT Afrika kuwa kuuawa kwa jamaa yake huyo kimeacha kovu kubwa kwa maisha ya jamaa zake.

“Baba yangu mdogo alikuwa hajamaliza hata miezi mitatu tangu kufunga ndoa alipouawa. Bibi yangu aliye jaa huzuni kubwa alimuomboleza kwa zaidi ya miaka 20, hadi alipokufa. Naye baba ambaye alimpenda kaka yake aliathirika sana na kifo cha ndugu yake. Hadi leo hatujui maiti yake ilizikwa wapi,” amesema Hazem.

“Ufaransa imekataa kukiri uhalifu wake dhidi ya raia wa Algeria, wala haitaki kututaka radhi,” aliongeza.

Ushawishi unafifia

Waandishi wa historia wameelezea kuwa ufaransa, ambayo iliitawala Algeria, iliingiwa na wasiwasi kwa kufifia ushawishi wake duniani katika miaka hiyo ya 1940.

Kuongezeka idadi ya waisalmu waliozaliwa nchini Algeria kulisababisha kuongezeka wito wa kurejeshwa umiliki wa ardhi kwa wenyeji wa Algeria na kuzidi wito wa kujitawala, na hivyo kuisukuma Ufaransa kuchukua hatua hiyo mwaka 1945.

Wazalendo wa Algeria, hasa katika miji ya Sétif na Guelma, walifanya maandamano dhidi ya utawala wa kifaransa mwaka 1945 ambayo yaliishia kwa umwagaji damu wiki mbili baadaye.

Mnamo Mei 8, Saal Bouzid, mwenye umri wa miaka 14, aliyekuwa mwanachama wa Muslim Scout, alipobeba bendera ya Algeria, Wafaransa, kufuatia amri kutoka kwa jenerali wa jeshi, waliwafyatulia risasi waandamanaji na kumuua Bouzid na wengine wengi

Maelfu ya maiti zilitapakaa kiasi kuwa ilikuwa vigumu kuzika. Hatimaye wengi wao walirushwa milimani au kutumbukizwa ndani ya visima.

Ghasia hizo ziliendelea hadi Mei 22 pale raia wa Algeria walijisalimisha.

Kufikia wakati huo, raia 45,000 wa Algeria wakiwemo wanawake na watoto, kutoka miji ya Setif, Guelma na Kherrata walikuwa wameuawa wakiwemo pia raia 100 wa Ufaransa, wengi wao wanajeshi.

Hata hivyo maandamano dhidi ya utawala wa kikoloni yaliendelea. mnamo Novemba 1954, Algeria ilirejelea kampeni yake kupigania uhuru. Juhudi zao zilifanikiwa hatimaye mnamo Juni 5 1962, pale Algeria ilipotangazwa kuwa taifa huru.

‘Maafa yasiyokubalika’

Kila mwaka, May 8, Algeria huadhimisha siku ya maombolezi ambayo hutofautiana sana na sherehe zinazofanyika kwingineko Ulaya.

Manmo Februari 27, 2005, aliyekuwa wakati huo balozi wa Ufaransa nchini Algeria, Hubert Colin de Verdière, aliomba msamaha rasmi kwa mauaji hayo ya halaiki, akiyataja kama ''maafa yasiokubalika ''.

Mnamo Mei Algeria kupitia Abdelmadjid Tebboune alisema kuwa “mauaji hayo ya kinyama'' yaliyofanywa wakati wa utawala wa kikoloni wa Ufaransa'' hayatosahaulika kamwe.''

Katika hotuba yake ya maadhimisho ya 77, ya mauaji hayo ya Mei 8, 1945, Tebboune alisema kuwa mauaji hayo yali badilisha kabisa historia ya taifa hilo.

Macron 'aomba radhi’

Mnamo Oktoba 17, 1961, wakati wa maandalizi ya uhuru wa Algeria, raia wengi zaidi waliadhibiwa na maafisa wa Ufaransa.

Polisi waliwashambulia takriban raia 25000, wazalendo wa chama cha Ukombozi wa Taifa (FLN) wakati wa marufuku ya kutoka nje ililiyo tangazwa dhidi ya raia wa Algeria.

Mnamo Oktoba 16, 2021, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliomba radhi kwa mashambulio ya 1961, akisema kuwa maandamano ya raia wa Algeria yalizimwa ''kikatili na kwa umwagaji damu.''

Rais huyo alisema ''anatambua ukweli: kuwa uhalifu uliofanywa siku hiyo chini ya uongozi wa Maurice Papon hayawezi kubalika nchini humo”.

kwa miaka mingi Algeria imekuwa ikiitaka Ufaransa kukiri makosa na kuwalipa fidia kwa ukatili uliofanyiwa raia wa nchi hiyo wakati wa utawala wa kikoloni wa Ufaransa kati ya mwaka wa 1830 na 1962.

TRT Afrika