Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Nelson Chamisa alipinga kuchaguliwa tena rasmi kwa Rais Emmerson Mnangagwa na kudai kuwa ameshinda.
Mnangagwa, 80, alishinda muhula wa pili kwa asilimia 52.6 ya kura dhidi ya asilimia 44 ya mpinzani wake mkuu, Chamisa, 45, kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa Jumamosi na Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC).
Chama cha upinzani cha Citizens Coalition for Change (CCC) kilikataa kuidhinisha matokeo hayo kikidai kuwa ya "uongo".
"Tumeshinda uchaguzi huu. Sisi ni viongozi. Tunashangaa hata kwa nini Mnangagwa ametangazwa kuwa kiongozi," Chamisa, wakili na mchungaji anayeongoza CCC, aliuambia mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu Harare
Raia wa Zimbabwe walipiga kura Jumatano na Alhamisi kumchagua rais na bunge jipya, katika upigaji kura uliokumbwa na ucheleweshaji uliozua shutuma za upinzani za wizi wa kura na kukandamizwa wapiga kura.
"Tulijua tunaingia kwenye uchaguzi wenye dosari. Tuna orodha ya wapigakura yenye dosari, ripoti yenye dosari. Tulikuwa na kura yenye dosari. Yalikuwa mazingira ya uchaguzi yenye dosari," Chamisa alisema.
Mapema katika ikulu ya rais Mnangagwa alitoa changamoto kwa waliopinga kuchaguliwa tena kwenda mahakamani. “Wale wanaohisi mbio hizo hazikuendeshwa ipasavyo wajue pa kwenda,” alisema.
Kura hiyo imetazamwa kote kusini mwa Afrika kama kipimo cha uungaji mkono wa chama cha Mnangagwa cha ZANU-PF, ambacho utawala wake wa miaka 43 umeambatana na uchumi unaodorora na madai ya ubabe.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alionyesha wasiwasi wake siku ya Jumapili kuhusu "kukamatwa kwa waangalizi, ripoti za vitisho vya wapiga kura, vitisho vya ghasia, unyanyasaji na kulazimishwa."
Guterres alitoa taarifa na kuzitaka pande zote "kusuluhisha kwa amani mizozo yoyote kupitia njia zilizowekwa za kisheria na kitaasisi" na kutatua mizozo "kwa njia ya haki, ya haraka na ya uwazi ili kuhakikisha kuwa matokeo yanaakisi mapenzi ya wananchi".
Waangalizi wa kigeni walitangaza Ijumaa kuwa uchaguzi umeshindwa kuendana na viwango vya kikanda na kimataifa.