Mchungaji mwenye ushawishi nchini Uganda na mfuasi mkubwa wa Rais Yoweri Museveni amelazwa hospitali baada ya kushambuliwa kwa risasi katika shambulizi ambalo limesababisha kifo cha mlinzi wake, polisi imesema.
Aloysius Bugingo alipigwa risasi Jumanne jioni pindi 'watu wasiojulikana walipoilenga gari yake kwa kutumia risasi za moto, kabla ya kukimbia kwa kutumia pikipiki," Polisi nchini Uganda imesema Jumatano.
Imesema uchunguzi umeanzishwa kuhusiana na 'jaribio hilo la mauaji ya mchungaji Aloysius Bugingo...na mauaji ya mlinzi wake, Muhumuza Richard."
Bugingo anafahamikwa kama mtu mtata nchini Uganda, ambapo ni kiongozi wa kanisa la House of Prayer Ministries — moja ya makanisa ya Pentecostal yenye ushawishi mkubwa katika eneo hilo la Afrika Mashariki.
Pia anamiliki vituo vyake vya runinga na radio, ambavyo anavitumia kuonyesha uungaji wake mkono kwa Museveni, ambae amekuwa madarakani tangu 1986.
Anaendelea kupata matibabu
"Licha ya kujeruhiwa katika shambulizi hilo, Mchungaji Aloysius Bugingo aliweza kuendesha gari mpaka Hospitali ya Mulago," polisi imesema.
"Kwa bahati mbaya, mlinzi wake, Muhumuza Richard, amekufa kutokana na shambulizi hilo pindi alipofika hospitali."
Wamesema, Bugingo "anaendelea na matibabu, na yuko chini ya uangalizi wa karibu."
Uungaji mkono wa Bugingo kwa rais, na zaidi kwa mtoto wake ambae anaonekana kama ndio mrithi wake, mara nyingi huwakasirisha wapinzani, ambao mchungaji anawakosoa wazi wazi katika mahubiri yake.