Spika wa Bunge la Uganda Anita Among. Picha Bunge la Uganda. 

Spika wa Bunge la Uganda Anita Among, amesisitiza kuwa Bunge la nchi hiyo litaanza kuendesha vikao yake katika mikoa minne tofauti ya nchi, kuanzia Kaskazini mwa Uganda kati ya Agosti 28 na 30, 2024.

Uamuzi huo umezua mjadala hasa kwa upande wa upinzani ambao umedai kuwa utaratibu huo utagharimu pesa nyingi, huku wananchi wakihofia kuwa bunge linapanga kutumia fedha nyingi katika kuendesha mikutano hiyo.

"Sidhani tunatumia bilioni 5 kwa kufanya mkutano ambao utakuwa katika eneo nje ya Kampala, kama vyombo vya habari vinavyosema. Sheria ya Bunge inamruhusu Spika kuamua mahali popote ambapo bunge linaweza kuketi," Naibu Spika wa Bunge Tayebwa amesema.

Msemaji wa Bunge Chris Obore amesema madai kwamba bunge litatumia fedha nyingi ni propaganda.

Kuanzia hasa baada ya msimu ya Uviko-19, ikiwa Rais Yoweri Museveni lazima ahudhurie bunge, kikao hufanywa katika maeneo ya wazi/ Picha: Bunge Uganda 

"Hakuna bajeti maalumu ya vikao vya mikoa. Kila kitu kinafanyika ndani ya mgao wa Bunge katika bajeti ya taifa. Kila kamati na idara ya bunge ina bajeti ya mwaka. Tunafanya kazi ndani ya hiyo bajeti. Mengine ni propaganda," Obore amesema kupitia akaunti yake ya X.

Enock Nyongore Mbunge wa Kaunti ya Nakaseke Kaskazini anaunga mkono uamuzi huo. Anasema utasaidi wananchi kuelewa mpangilio wa majadiliano bungeni.

"Mikutano ya mikoa ni wazo zuri, tukiwa katika mikoa fulani tutaangalia changamoto za eneo hilo lijadiliwe na watu watajionea moja kwa moja jinsi bunge linavyojadili na serikali inajibu," Nyongore amesema.

Joel Ssenyonyi, kiongoiz wa upinzani, anasema shida za amaeneo zinaweza kutatuliwa bila ya bunge zima kwenda huko.

"Kusafirisha bunge zima na wanafanyakazi wake itakuwa gharama kubwa, cha muhimu inafaa kuzipa kipaumbele changamoto za eneo la kaskazini mwa Uganda ambayo tunajua wazi.

Spika wa Bunge amesisitiza kuwa itakuwa muhimu kwa bunge kutembea katika mikoa tofauti ya nchi kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika majadiliano ya changamoto wanazohitaji kutatuliwa na serikali.

Haitakuwa mara ya kwanza bunge kuhamisha vikao vyake.

Kuanzia hasa baada ya msimu ya Uviko-19, ikiwa Rais Yoweri Museveni lazima ahudhurie bunge, kikao hufanywa katika maeneo ya wazi.

TRT Afrika