Baraza la Mawaziri lililoteuliwa na Rais wa Rwanda paul Kagame linaapishwa Jumatatu, Agosti 19, na hapo kuashiria mwanzo wa kazi ya serikali katika muhula wa miaka mitano ujao wa Rais Kagame.
Kagame alitangaza baraza lake jipya ijumaa baada ya kumteua tena Edouard Ngirente kuwa Waziri Mkuu.
Mawaziri kadhaa waliokuwa ofisini kabla ya Rais Kagame kushinda muhula mwingine katika uchaguzi wa Julai wameteuliwa tena.
Miongoni mwa sura mpya katika Baraza la Mawaziri ni Prudence Sebahizi, Waziri mpya wa Biashara na Viwanda na Richard Nyirishema, Waziri wa Michezo, na Christine Nkulikiyinka, Waziri wa Utumishi wa Umma na Kazi.
Pia kuna Doris Uwiceza Picard aliyechaguliwa kama Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utawala ya Rwanda (RGB).
Kabla ya uteuzi wake, Sebahizi, mwanauchumi wa biashara aliyechukua nafasi ya Jean Chrysostome Ngabitsinze, alikuwa Mkurugenzi wa Uratibu wa Masuala ya Kitaasisi na Uratibu wa Programu katika Sekretarieti ya Eneo Huria la Biashara la Afrika (AfCFTA) mjini Accra, Ghana.
Sebahizi alikuwa sehemu ya mazungumzo yaliyopelekea Rwanda kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 2007. Pia amewahi kuishauri serikali ya Rwanda kuhusu ushirikiano wa kikanda.
Hadi kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma na Kazi, akichukua nafasi ya Jeanne d’Arc Mujawamariya ambaye alifutwa kazi mwishoni mwa Julai, Nkulikiyinka alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la 'Rwanda Cooperation Initiative'.
Hapo awali aliwahi kuwa balozi wa Rwanda katika nchi za Nordiki, mjumbe kwa Ujerumani, na Urusi. Nyirishema, ambaye alichukua nafasi ya Aurore Mimosa Munyangaju, alikuwa makamu wa rais wa mashindano katika Shirikisho la Mpira wa Kikapu la Rwanda (FERWAFA), nafasi ambayo alikuwa ameshikilia tangu 2016.