Kuanzia Septemba 2023 hadi Februari 2024, kumekuwa na ongezeko la mavuno la tani 316,000 za mavuno nchini Rwanda  / Picha : Wizara ya kilimo Rwanda 

Rwanda imepata ongezeko la uzalishaji wa kilimo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa 2024.

Kuanzia Septemba 2023 hadi Februari 2024, kumekuwa na ongezeko la tani 316,000 za mavuno ikilinganishwa na mwaka uliopita. Hii ni kulingana na Bodi ya Maendeleo ya Kilimo na Rasilimali ya Wanyama ya Rwanda (RAB).

Rwanda imeripoti kuongezeka kutoka tani 4,063,804 msimu wa 2023 hadi tani 4,379,725 msimu wa awali wa 2024.

Mkurugenzi Mkuu wa RAB, Telesphore Ndabamenye, alibainisha kuwa kulima kwenye ardhi ambayo awali ilikuwa haitumiki kumechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uzalishaji msimu huu.

“Aina hii ya ardhi ilipatikana hasa katika wilaya za Nyagatare, Gatsibo, Kayonza na Kirehe, ambapo wakulima walitenga sehemu kubwa kwa ajili ya ufugaji wa ng’ombe ili kuongeza uzalishaji," Ndabamenye alieleza.

Katika msimu wa mazao wa kwanza wa 2024, serikali ilisema asilimia 7.5 ya wakazi walitumia kilimo cha umwagiliaji kuongeza uzalishaji.

Mwenyekiti wa Ushirika wa Wakulima wa Mpunga katika wilaya za Ngoma na Kirehe Evariste Harerimana anasema hii imechangia mazao bora.

Ameelezea asilimia 90.6 ya wakulima walipitisha mitaro ya kuzuia mmomonyoko wa udongo, huku wengine wengi wakipokea msaada wa serikali kutengeneza na kutekeleza matuta katika mikoa mbalimbali.

Kwa kuandaa mitaro kuelekeza maji kwenye mazao yao, walifanikiwa kuongeza uzalishaji wa vyama vyao vya ushirika kutoka tani 2,400 hadi tani 2,800.

Mazao haya bora yanakuja huku Rwanda ikijitayarisha kwa sherehe ya chakula inayoitwa "Umuganura."

Siku ya Umuganura ni sherehe kubwa nchini Rwanda na huadhimishwa Ijumaa ya kwanza ya mwezi Agosti kila mwaka. Ni sikukuu ya umma nchini Rwanda na pia inajulikana kama siku ya kitaifa ya mavuno kwani inaadhimisha mwanzo wa msimu wa mavuno.

TRT Afrika