Raia wa Mauritius hawataweza kutumia mitandao ya kijamii hadi Novemba 11, siku moja baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo./ Picha: Getty 

Mamlaka ya mawasiliano ya Mauritius ilisema siku ya Ijumaa kwamba watoa huduma zote za intaneti lazima wasitishe upatikanaji wa mitandao ya kijamii hadi Novemba 11, siku moja baada ya uchaguzi mkuu ujao, huku nchi ikikumbwa na kashfa ya udukuzi wa mawasiliano.

Mazungumzo kadhaa yanayowahusisha wanasiasa, polisi, mawakili, waandishi wa habari, na wanachama wa jamii yamevuja kwenye mitandao ya kijamii tangu katikati ya mwezi wa Oktoba, kulingana na shirikla la uangalizi wa vyombo vya habari la Reporters Without Borders.

Katika uchaguzi wa Novemba 10, Waziri Mkuu Pravind Kumar Jugnauth anatafuta kudumisha wingi wa chama chake cha Militant Socialist Movement (MSM) bungeni na kujipa miaka mingine mitano madarakani.

Jugnauth na polisi wamedai kwamba mazungumzo ya simu yaliyovuja yamebadilishwa kwa kutumia teknolojia ya akili mnemba.

TRT Afrika