Idara ya Ofisi ya Hazina ya Udhibiti wa Mali za Kigeni ya Marekani (OFAC), imetangaza kumuwekea vikwazo Abdel Fattah Al-Burhan, kiongozi wa Kikosi cha Wanajeshi wa Sudan (SAF).
"Hatua ya leo inasisitiza dhamira yetu ya kuona mwisho wa mzozo huu," Naibu Katibu wa Hazina Wally Adeyemo alisema katika taarifa.
Al Burhan pia ni Rais wa Baraza la Mpito la Sudan.
Vita nchini Sudan kati ya jeshi la Sudan na kikundi cha Rapid support Forces vinaendelea tangu Aprili 2023.
"Marekani itaendelea kutumia zana zetu kuzuia mtiririko wa silaha nchini Sudan na kuwawajibisha viongozi hawa kwa kutojali maisha ya raia."
Marekani inasema jeshi chini ya uongozi wa al Burhan limefanya mashambulizi mabaya kwa raia, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya anga dhidi ya miundombinu inayolindwa ikiwa ni pamoja na shule, masoko na hospitali.
Marekani imesema jeshi pia limezuia kwa makusudi ufikaji wa misaada ya kibinadamu, na kutumia mbinu ya kuwanyima watu chakula kama silaha.
Hatua hii inafuatia siku chache baada ya Marekani kumuwekea vikwazo kiongozi wa Rapid Support Forces (RSF), Mohammad Hamdan Daglo Mousa (Hemedti), Januari 7, 2025.
Aidha, OFAC imeweka vikwazo pia kwa kampuni moja na mtu mmoja anayehusika na ununuzi wa silaha kwa niaba ya Mfumo wa Viwanda vya Ulinzi (DIS), kitengo cha ununuzi cha jeshi la Sudan.
Ahmad Abdalla (Abdalla) ni raia wa Sudan-Ukraine na afisa wa Mfumo wa Sekta ya Ulinzi (DIS), kitengo kikuu cha manunuzi cha jeshi la SAF.
Tangu OFAC ilipoweka vikwazo Juni 2023, kampuni hiyo imetafuta silaha na vifaa vyengine kupitia njia zisizo rasmi.
Vikwazo vinahusisha nini?
"Kutokana na hatua ya leo mali yote ya watu walioteuliwa walioelezwa hapo juu iliyo Marekani au katika milki au udhibiti wa watu wa Marekani imezuiwa na lazima iripotiwe kwa OFAC," Marekani imesema.
Kwa kuongezea, biashara au mali zozote zinazomilikiwa, moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja, binafsi au kwa jumla, kwa asilimia 50 au zaidi na waliowekewa vikwazo, vitazuiliwa.
"Vikwazo vya Marekani kwa ujumla vinakataza shughuli zote za watu wa Marekani au ndani ya Marekani ambazo zinahusisha mali au maslahi yoyote katika mali ya watu waliowekewa vikwazo," Marekani imesema.