Donald John Trump alizaliwa huko Queens, New York, Juni 14, 1946.
Baba yake, mwekezaji mkubwa katika ujenzi na nyumba akifanikiwa kuwa tajiri wa mali isiyohamishika. Trump alisoma katika Chuo cha Kijeshi cha New York na Shule ya Fedha na Biashara ya Wharton katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania. Mnamo 1971, alirithi kampuni ya baba yake, akiita Shirika la Trump.
Biashara hii hivi karibuni ilijihusisha katika miradi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na hoteli, majengo ya makazi na biashara, kasino na viwanja vya gofu. Kitabu chake cha kwanza kati ya vitabu vingi kilikuwa The Art of the Deal, kilichochapishwa mwaka wa 1987.
Mnamo 2004, alizindua kipindi cha televisheni cha The Apprentice. Mnamo 2005, Donald Trump alifunga ndoa na Melania Knauss.
Wana mtoto mmoja wa kiume, Barron. Trump pia ana watoto wanne wengine kutoka kwa ndoa za awali: Donald Jr., Ivanka, Eric na Tiffany.
Wakati wa kura za mchujo wa 2016, Trump aliwashinda zaidi ya wapinzani kumi na kushinda uteuzi wa Republican.
Japo alipoteza kura ya umaarufu ya wananchi, Trump alimshinda aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje Hillary Clinton katika uchaguzi mkuu kwa kupata kura nyingi za Chuo cha Uchaguzi.
Kauli mbiu yake ya kampeni ilikuwa “Irudishe Marekani katika hadhi yake.”
Ulikuwa ushindi uliowaacha wengi na butwaa kwani japo walimuona kuwa ni mtu anayetafuta tu sifa mtandaoni na mwenye kashfa zilizomzunguka kwamba hangeweza kushinda lakini haswa ndiyo yaliyompa ushindi.
Bila uzoefu wa kisiasa uliochaguliwa hapo awali, Rais Trump alitumia njia zisizo za kawaida kuwasilisha vipaumbele vyake. Hasa zaidi, alitumia jukwaa la kijamii la Twitter kama njia kuu ya mawasiliano ya moja kwa moja na umma wa Marekani, wanasiasa wengine, na vyombo vya habari.
Akiwa Rais, alitia saini muswada mkuu wa marekebisho ya kodi kuwa sheria na akasimamia kupunguzwa kwa kanuni za shirikisho. Katika sera ya mambo ya nje, utawala wa Trump ulihamisha Ubalozi wa Marekani nchini Israel kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem na kuratibu mikataba ya kuhalalisha uhusiano kati ya Israel na nchi kadhaa.
Mnamo mwaka wa 2018, Rais Trump alihudhuria mkutano na Kim Jong Un, ikiwa ni mara ya kwanza kwa rais aliyekuwa madarakani kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini.
Mnamo mwaka wa 2018, serikali nusura ilikwama kuendelea kwani Trump hakukubaliana na Congress juu ya ufadhili wa ukuta wa mpaka kati ya Marekani na Mexico.
Ukosefu wa ufadhili ulichukua siku 35 kabla ya kutatuliwa. Mnamo mwaka wa 2019, Baraza la Wawakilishi lilimshtaki Rais Trump kutokana na madai ya kuzuia Bunge la Congress na matumizi mabaya ya madaraka.
Mnamo 2020, Seneti ilimwachilia Trump kwa vifungu vyote viwili vya mashtaka. Kesi ya kwanza iliyothibitishwa ya COVID-19 iliripotiwa nchini Marekani mnamo Januari 20, 2020.
Sehemu iliyobaki ya urais wa Trump iliharibiwa na janga la coronavirus.
Wengi walikosoa namna Trump alivyoshughulikia janga la COVID akichangia watu kukosa kupata chanjo na kuvaa barakoa.
Kufikia wakati Trump anaondoka madarakani, zaidi ya Wamarekani 400,000 walikuwa wamekufa kwa COVID-19. Uchaguzi uliopita Trump alipambana na Joe Biden na mnamo Januari 6, 2021, kwa mara ya kwanza matokeo ya uchaguzi yakakumbwa na rabsha kupelekea wafuasi wake kuvamia majengo ya bunge na kusababisha vurugu.
Trump amefunguliwa mashtaka 13 kwa jumla huku matano yakifutwa na mengine yakiwa yanaendelea kusikilizwa au kusubiri hukumu.
Ndiye Rais pekee katika historia ya Marekani kushtakiwa na kupigiwa kura ya kuondolewa mara mbili na Bunge la Congress.