NA DAYO YUSSUF
Falsafa ya mwandishi wa Uingereza George Orwell inasema kwamba "njia bora zaidi ya kupotosha watu ni kukataa na kufuta uelewa wao wenyewe wa historia yao".
Msururu wa habari kuhusu milipuko, milio ya risasi na moshi unaofuka kutoka kwa majengo katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, unaibua hofu hiyo hiyo kwa Agnes Kinyua, mhadhiri wa historia aliyebobea katika ustaarabu wa dunia katika Chuo Kikuu cha Strathmore nchini Kenya.
Anapofuatilia vita vya wenyewe kwa wenyewe katika taifa hilo la Afrika, hofu yake kubwa ni historia - vitabu, kazi za sanaa na makumbusho yote - kupata hasara kubwa zaidi katika ghasia.
"Nimekuwa nikiwatazama," Agnes anasema kuhusu wale waliohusika katika mapigano hayo. "Wanapochoma vitabu, hawajali. Wanachoma kila kitu, wanaiba, na wanaharibu. Mbali na vitu vya kale, tuna kumbukumbu za kihistoria huko Sudan. Ni wasiwasi kwangu, na nina uhakika kwa mtu mwingine yeyote anayejali historia. ."
''Bila dalili ya mzozo kuisha, wasiwasi huu unaonekana kukita mizizi. "Wakati vitu vyetu vya sanaa vimetoweka, tutakuwa na taarifa zisizo za ukweli. Historia itapotea," Agnes anaiambia TRT Afrika.

Gharama ya migogoro, hasa ya ndani, ni mojawapo ya aina zisizo na mpangilio na zisizotabirika za uharibifu.
Gharama ya vita
Ni itikadi ambapo kila mmoja ajipiganie kuinusuru nafsi yake.
Kuna matukio yaliyorekodiwa ya vikundi vilivyo katika mzozo kuzidi ushari wao na kutumia watu kama ulinzi, biashara ya mazungumzo, au hata silaha za vita. Masalia ya zamani, ikiwa ni pamoja na mambo ya kale na makaburi, ambayo yanaunda historia ya taifa au ustaarabu pia hutokea kuwa miongoni mwa walengwa walio hatarini zaidi katika mzozo.
"Ni muhimu kuelewa umuhimu wa vitu vya kale. Huwezi kuharibu mabaki muhimu ya kihistoria ili kuonyesha hasira au kuadhibu kundi pinzani," anasema Agnes.
Tangu mapigano yazuke nchini Sudan katikati ya mwezi wa Aprili, ripoti zimeibuka kutoka Khartoum kuhusu miganda ya nyaraka za kihistoria kuchomwa na kuwa majivu pamoja na vitabu.

Ripoti ya shirika lisilo la kiserikali la Heritage for Peace, inayofanya kazi ya kuhifadhi historia nchini Sudan, mwishoni mwa mwezi Aprili ilisema idadi kubwa ya vito vya kale katika makumbusho ya historia ya asili huko Khartoum iliharibiwa kwa moto.
‘"Makumbusho hayo, ambayo ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Khartoum, yalihifadhi mkusanyiko wa mimea adimu, vielelezo vya viumbe vilivyotoweka nchini Sudan, pamoja na wanyama na wadudu (takriban vielelezo 100)," inasema ripoti hiyo. "Kwa bahati mbaya, mkusanyiko ulipotea, na jengo lenyewe liliharibiwa vibaya."
Jumba la makumbusho lililo katikati mwa Khartoum liko katika eneo la kijeshi la Sudan, na kwa sasa raia wa kawaida wamepigwa marufuku eneo hilo.
Kumekuwa na kushutumiana kati ya pande zinazozozana kuhusu nani anahusika kuharibu mikusanyiko yenye umuhimu wa kihistoria.
Kikosi cha Wanajeshi wa Msaada wa Haraka (RSF), ambacho kinapigana dhidi ya jeshi, kilipiga picha ya video Jumba la Makumbusho la Kitaifa mwanzoni mwa Juni kwa video, ambapo kilionyesha masanduku yaliyo na vitu vya sanaa vikiwa vimehifadhiwa pamoja na maiti zilizotiwa mumiani na nyaraka zilizohifadhiwa kwa usalama.

RSF ilipuuzilia mbali ripoti za "uongo na habari zisizofaa" kuwa wanachama wake walihusika katika uharibifu wa taasisi za kiakiolojia na za kihistoria.
Vyovyote vile, ukweli unabakia kuwa ushahidi mwingi wa ustaarabu wa siku za nyuma umeharibiwa tayari. Wale kama Agnes wana wasiwasi kwamba kama hakuna kitakachofanyika kuhusu hilo, Sudan itapoteza mengi zaidi.
Heritage for Peace inasema kwamba angalau maeneo 28 ya kitamaduni na kiakiolojia kote nchini yamelengwa, au yamepata uharibifu fulani.
Nafasi ya Sudan katika historia
Umuhimu wa Sudan katika historia ya ustaarabu wa Mashariki na Kaskazini mwa Afrika hauwezi kupuuzwa.
Kuchipua kutoka katikati ya nchi ambapo mito miwili mikuu hukutana - Blue Nile na White Nile - Ufalme wa Kush ulijulikana kwa biashara ya dhahabu na chuma. Ilikuwa pia njia muhimu kati ya falme za kaskazini na kusini mwa Sahara.

Kisha kuna piramidi na makaburi ambayo yanaashiria alama za uhusiano wa eneo hilo na jirani yake wa kaskazini, Misri.
Mzunguko huu wote wa historia unaoanzia mwaka wa 1070 (Kabla ya Kristu) uko katika hatari ya kuangamizwa ikiwa hakuna mtu atakayesimama kuulinda huku kukiwa na ufyatuaji risasi na mabomu nchini Sudan.
"Hii haihusu Sudan pekee," anasema Agnes. "Wakati wa vita au msukosuko wowote kama huo, watu wengi husahau maeneo ya makumbusho."
Somalia, nchi yenye historia na utamaduni tajiri, ni mojawapo ya mifano hiyo ndani ya bara.
"Vitu vingi vya kale vimepotea kwa miaka mingi ya migogoro. Sasa, tunajitahidi kuunganisha historia na utamaduni wa eneo hili, na kuihifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo. Hatupaswi kuruhusu yaliyotokea Somalia kutokea Sudan, au hata Magharibi mwa Afrika,” anaonya Agnes.
''Wahifadhi wanapaswa kupigana kulinda vitu vya kale. Wanapokimbilia usalama pamoja na familia zao, wanaweza kuleta vitu hivi vya kale vya thamani, kama wanaweza,'' anaongeza Agnes,

Wataalamu wa mambo ya kale nchini Sudan wanasema wamekuwa wakihangaika kuokoa wanachoweza tangu mapigano yalipozuka.
''Tunajaribu tuwezavyo kuhakikisha kuwa makaburi haya, sanaa na vitu vya sanaa ni salama. Tunataka kuhakikisha kuwa yanajulikana kwa kila mtu," anasema Ibrahim Musa, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kitaifa la Mambo ya Kale na Makumbusho la Sudan.
Agnes anapendekeza kuongeza majukumu ya vikosi vya kulinda amani ili kujumuisha ulinzi wa vito hivi vya kale.
"Umoja wa Mataifa unaweza kuingilia kati. Vivyo hivyo na shirika lingine lolote lenye mamlaka kama vile Umoja wa Afrika au ECOWAS. Wanaweza kusaidia kutoa usalama, au angalau kusaidia katika kupeleka vitu hivi vya kale kwenye maeneo salama," anasema.
Kulingana na Heritage for Peace, angalau makumbusho manne katika eneo la Magharibi mwa Darfur yameharibiwa, ikiwa ni pamoja na Makumbusho maarufu ya Nyala, ambayo paa lake lililipuliwa kwa makombora, na kuhatarisha uharibifu zaidi wa mambo ya ndani kutokana na kuvuja kwa maji ya mvua.

Sudan ina angalau makumbusho sita makubwa na mengine mengi madogo yaliyotawanyika kote nchini.
UNESCO imeorodhesha maeneo mawili nchini Sudan kama maeneo ya Urithi wa Dunia: Kisiwa cha Meroe, nyumbani kwa moja ya majengo makubwa ya kale ya piramidi barani Afrika, na Jebel Barkal, mlima mtakatifu wa mchanga ulio karibu na makaburi, mahekalu na majumba kando ya Mto Nile.
NakKila wakati bomu linapolipuka na jengo kuharibiwa katika mzozo unaoendelea, Agnes na wenzake wapenzi wa hhistoria hiungiwa na wasiwasi juu ya usalama wa vito vya kale.