Maouvu yasiosahaulika ya Ubelgiji kwa Wakongomani enzi za Ukoloni

Maouvu yasiosahaulika ya Ubelgiji kwa Wakongomani enzi za Ukoloni

Licha ya Mfalme wa Ubelgiji kusema anajutia maovu Wabelgiji waliwatendea Wakongomani enzi za ukoloni, wapo watu wengi tu wanaohisi kuwa kauli yake sio ya kuomba msamaha kwa machafu Ubelgiji iliyafanya nchini DR Congo enzi za ukoloni.

Mfalme Philippe wa Ubelgiji hajaomba radhi kwa vitendo vya unyanyasaji, ubaguzi wa rangi na vitendo vya ukatili vilivyoelekezewa Wakongomani. Hatahivyo Mfalme huyo alisema kuwa anajutia vitendo na maovu hayo yaliyofanya na mababu zake.

Philippe ambaye alirithi Ufalme mwaka 2013 ni Mkuu wa kwanza kutoka Ubelgiji kufichua kuwa anajutia vitendo vya Ubelgiji enzi za ukoloni lakini Wakongomani wengi wanasema kuwa walitarajia kuwa Mfalme huyo atatoa msamaha rasmi kwa DR Congo.

“Licha ya kuwa Wabelgiji wengi waliwekeza kiukweli kwa kuipenda Congo na watu wake, utawala wa wakoloni uliendeshwa kwa unyanyasaji mkubwa.” Mfalme Philippe aliambia kikao cha pamoja cha Bunge katika jijini Kinshasa, DRC.

“Utawala wa enzi hizo haukuzingatia usawa na haki za Wakongomani na ulitawala kwa ubaguzi wa rangi.”

“Hili lilipelekea kuwepo kwa vitendo vya ukatili na vya kudhalilisha. Katika ziara hii yangu ya kwanza hapa Congo na mbele ya Wakongomani na wale wangali na maumivu, napenda kusema kuwa najutia sana maovu hayo.” Mfalme huyo aliongeza.

Lakini licha ya Mfalme Phillipe kuonesha mwanzo wa kukiri machafu ya Ubelgiiji enzi za ukoloni, wapo wengi wanaohisi majuto yake sio sawa na kuomba msamaha kama ilivyotarajiwa na wengi.

Haya hapa ni baadhi tu ya maovu Wabelgiji waliwafanyia Wakongomani enzi hizo za ukoloni:

Vifo vya Wakongomani milioni 10

Kwa mujibu wa makadirio, takriban watu milioni 10 waliaga dunia kutokana na kuuliwa, ukame na magonjwa chini ya utawala wa Mfalme Leopold II nchini humo kati ya 1885 na 1960. Mfalme huyo alijinyakulia ardhi kubwa akidai ni kwa ajili ya kuwasitiri Wabelgiji kutoka kwa watumwa wa Uarabuni.

Ubakaji na mateso

Mfalme Leopold II aligeuza mashamba makubwa ya Wakongomani kuwa kambi za kazi na vibarua vigumu kwa lengo la kujizolea utajiri.

Nguvu ya kazi ya ukulima ilitokana na kulazimishwa kazi kwa Wakongomani huku wenyeji wakiendelea kusota kwenye ufukara mkubwa ndani ya tiafa lao.

Aidha Wakongomani wengi walibakwa na kuteswa nyakati hizo.

Mfalme Leopold II aliwatesa Wakongomani kwa kukata miguu na mikono yao hasa waliogoma kumtii na kufuata masharti ya utawala wake. Kadhalika wake na watoto wa wanaume waliogoma kumtii vilevile walifanyiwa ukatili uo huo.

Vitendo hivyo vya ukatili vilikuwa mbinu ya Wabelgiji ya kulazimisha utii miongoni mwa Wakongomani.

Maovu ya machafu haya yote yanaaminika kuanza mwaka wa 1885 na yalifichuliwa kwa mara ya kwanza na Mwanahabari Edmund Dene Morel mwanzoni mwa karne ya ishirini(20). Morel alijitahidi pakubwa kueneza habari juu ya maovu yalikuwa yakielekezewa Wakongomani mikononi mwa Wabelgiji.

Mwanahabari huyo alivujisha picha za kusikitisha zikionesha ukatili mkubwa, vifo, wanajeshi watoto, walemavu wasio na mikono na miguu.

Ikumbukwe mwaka 2020 sanamu ya Mfalme Leopold II iliharibiwa na waandamanaji Jijini Antwerp, Ubelgiji kwenye vuguvugu la maandamano ya kupinga maovu na machafu ya mataifa ya Magharibi enzi za Ukoloni.

Reuters