Ronald Sonyo
TRT Afrika, Dodoma, Tanzania
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini Tanzania-TAWA imekamilisha uchunguzi wake wa siku kadhaa baada ya shutuma nzito kuelekezwa kwa mamlaka hiyo kuhusu uhalali wa wawindaji wawili wa kigeni ambao ni wanandoa kumuua mamba mwenye umri wa miaka 100 katika mojawapo ya hifadhi ya wanyama nchini humo.
Vipande vya video vilivyosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii vilimuonesha mwindaji huyo akiwa na mamba aliyewindwa viliibua hisia na taharuki kubwa katika jamii. Hata hivyo, Disemba mwaka jana TAWA iliahidi kufanya uchunguzi zaidi juu ya hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TAWA imesema uchunguzi umebaini kuwa mamba aliyeonekana kwenye picha jongefu (video clip) iliyosambaa aliwindwa katika kitalu cha Lake Rukwa GR kwa kibali halali namba MP-0001792 kilichoanza tarehe 12/08/2023 hadi 09/09/2023.
Mnyama huyo alikuwa na urefu wa futi 16.2 sawa na sentimita 493.8 ikiwa ni juu ya kiwango cha chini cha urefu wa sentimita 300 unaohitajika kwa mujibu wa Sheria.
“kwa mujibu wa takwimu za taasisi ya Marekani (Safari Club International - SCI), mamba mrefu zaidi duniani aliwindwa nchini Ethiopia rnwaka 2005 (futi 18.7 sawa na sentimita 561)” ilifafanua taarifa hiyo.
“Umma unahakikishiwa kuwa uwindaji wa wanyamapori nchini unazingatia Sheria na taratibu za ndani ya nchi na zile za kimataifa na Mamlaka inawatoa hofu kuwa taratibu hizi zinasimamiwa ipasavyo na pale panapotokea ukiukwaji hatua stahiki huchukuliwa kwa mujibu wa sheria,” ilisema taarifa hiyo.
Hata hivyo taratibu za mkataba wa kimataifa wa CITES, Tanzania imeruhusiwa kuwinda mamba wasiozidi 1,600 kwa mwaka, taarifa hiyo imesema kuwa, mpaka sasa ni jumla ya mamba 39 tu kati ya hao waliowindwa kutoka kwenye mgawo (quota) wa Taifa wa mwaka 2023.
Itakumbukwa kwamba, hii sio mara ya kwanza kwa mamba kuuliwa, mwaka 2016, mamba mwenye uzito wa kilo 360 aliuwawa katika jimbo la Florida nchini Marekani baada ya kuleta uharibifu na kula n’gombe.