Watu wenye silaha waliowateka nyara takriban wanafunzi mia tatu kutoka shule moja katika jimbo la Kaduna, kaskazini mwa Nigeria wamewaachilia, mamlaka imetangaza.
Watoto hao walikamatwa katika mji wa Kuriga mapema mwezi huu wakati nchi hiyo ya Afrika Magharibi ikikabiliana na utekaji nyara ili kulipwa fidia na magenge yenye silaha.
''Ningependa kutangaza kwamba watoto wetu wa shule ya Kuriga wameachiliwa,'' gavana wa jimbo la Kaduna Uba Sani alisema katika taarifa Jumapili asubuhi.
'Siku ya furaha'
Wahasiriwa walikuwa wanafunzi wa shule ya msingi na wanafunzi wa shule ya upili wanaosoma katika kituo kimoja wakati watu wenye silaha walipovamia na kufyatua risasi.
Mamlaka haijatoa maelezo kuhusu jinsi wateka nyara waliachiliwa na ikiwa fidia ililipwa kwa watekaji nyara.
Lakini gavana Sani alisema ''watoto wa shule ya Kuriga waliotekwa nyara wanaachiliwa bila kudhurika.''
Serikali ya jimbo la Kaduna na serikali ya shirikisho ilibuni ''mikakati'' na kuratibu utendakazi wa mashirika ya usalama ambayo ''hatimaye ilisababisha matokeo haya yenye mafanikio,'' aliongeza.
''Hakika hii ni siku ya furaha,'' gavana huyo alisema.
Wahalifu wanaodhalilisha
''Jeshi la Nigeria pia linastahili pongezi maalum kwa kuonyesha kwamba kwa ujasiri, uamuzi na kujitolea, wahalifu wanaweza kudhalilishwa na usalama kurejeshwa katika jamii zetu,'' Sani alielezea.
Kuachiliwa kwa wanafunzi hao wa Kuriga kumekuja siku moja baada ya jeshi la Nigeria kuwaokoa kundi jingine la wanafunzi waliotekwa nyara na mwanamke mmoja katika jimbo la kaskazini magharibi la Sokoto.
Walitekwa nyara kutoka shule ya Qur'ani inayojulikana kama shule ya Tsangaya mnamo Machi 9, siku mbili baada ya kutekwa nyara kwa umati kwa watoto wa shule ya Kuriga.