Mambo gani yanafanya Afrika kuwa mahali bora pa kuishi kuliko Marekani?

Mambo gani yanafanya Afrika kuwa mahali bora pa kuishi kuliko Marekani?

"Ikiwa haujui ukweli halisi kuhusu Marekani, utadanganyika kukimbilia kule"
  Rick na mke picha:  Rick Family  

Na Abdulwasiu Hassan

Huu ni ujumbe kutoka kwa Mmarekani mwenye asili ya Afrika aliyechukua uamuzi wa ajabu wa kuacha kazi yake katika jeshi la Marekani na kuhamia taifa la Afrika Magharibi la Gambia ili kuwa mkulima.

Rick Devon Usumbura, ambaye alihamia barani Afrika yeye na familia yake mwaka 2016, anaiambia TRT Afrika kwamba anaamini Afrika ni mahali pazuri pa kuishi kuliko popote Ulaya na Marekani. Hii ni tofauti kabisa na mwenendo wa sasa wa uhamaji wa watu wengi kutoka Afrika kwenda Ulaya na Marekani, hasa kwa vijana wanaotafuta fursa bora zaidi.

Wahamiaji wengi haramu hutumia njia hatari kama Jangwa la Sahara na Bahari ya Mediterania katika harakati zao za kutafuta maisha mazuri. Kulingana na taasisi ya Save the Children, takriban watu nusu milioni walikuwa wamevuka au kujaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kwenda Ulaya tangu 2019.

Katika ripoti ya Februari mwaka huu, shirika hilo la misaada lilisema wahamiaji 8,468 ama walikufa au kupotea walipokuwa wakijaribu kuvuka bahari, wengi wao kwa boti. Maelfu ya wengine walifanikiwa kuingia Ulaya kihalali.

Rick, 59, anaamini kuwa kuna maisha bora barani Afrika kuliko kile ambacho wahamiaji wengi wanaoondoka barani humo wanategemea. Mara baada ya kuwasili Gambia, alinunua kipande cha ardhi na kuanzisha shamba lililoitwa “Shamba la Mtu Mweusi Gambia”.

Mkewe Cynthia na watoto wao wanne awali walikuwa wakipinga kukaa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, lakini aliweza kuwashawishi. Sasa hivi wote wanaishi vizuri na kwa furaha katika nchi ambayo inahesabiwa kuwa miongoni mwa vivutio kuu vya utalii katika eneo hilo.

"Jamani, nilikuwa nikitamani nyakati hizi maisha yangu yote, niweze kutembea kwenye ardhi yangu mwenyewe, sio kuruka uzio wa mtu," anaeleza Rick, huku akiuma kipande cha za tunda la nyota alilochuma kutoka kwenye mti mmojawapo shambani kwake.

Katika video iliyorekodiwa na mke wake na kupandishwa kwenye chaneli yao ya YouTube, Mmerikani-Mwafrika huyo, huku akiwa na uso wenye furaha, anaongeza kuwa sasa “naweza kula matunda mengi kadri nipendavyo".

'Ndoto ya fahari ya Umarekani' inapogeuka shubiri

Alizaliwa katika mji wa Dublin katika jimbo la Georgia la Marekani, na baadae akingali mtoto, Rick na wazazi wake walihama na kwenda kuishi Chicago nyakati za kile kinachoitwa ‘Uhamaji Mkuu’ ambapo karibu watu weusi milioni sita walihama kutoka vijijini kusini hadi kaskazini mijini katika karne ya 20.

Baada ya kuwa mtu mzima, Rick alijiunga na Jeshi la Marekani. Lakini baada ya miaka 15 hivi jeshini, alijiuzulu kama sajenti mkuu wa kikosi.

Rick anaiambia TRT Afrika kwamba aliacha kazi kutokana na kuzorota kwa afya na kutokuwa na uwezo wa kuendelea kukabiliana na "ubaguzi wa rangi wa kitaasisi". Aliendesha kampuni ya kusafisha nyumba nchini Marekani kabla ya kuhamia Gambia, Kusini mwa Jangwa la Sahara na familia yake.

Rick anakumbuka kwa kiasi fulani kuhamasishwa na msimamo wa Rais wa zamani wa Gambia Yahaya Jammeh, ambaye aliwataka Waafrika kufanya juhudi zaidi kujitosheleza katika uzalishaji wa chakula. "Sababu iliyotufanya tuamue kuhamia Afrika ni kwamba hakuna ya fahari ya kuwa Mmarekani. Ndoto iliyopo ni ya jinamizi tu," anasema.

Rick Gambia

Madai ya ubaguzi wa rangi kutuka kwa vikosi vya usalama vya Marekani yamekuwa yakijirudia katika miaka ya hivi karibuni, kuhusiana jinsi yanavyowatenda wanajeshi weusi pamoja na raia weusi. Tukio muhimu zaidi lilikuwa mauaji ya Mmarekani mweusi asiye na silaha, George Floyd, mnamo 2020 ambayo yalisababisha maandamano mitaani na kulaaniwa ulimwenguni kote.

Kufuatia tukio la Floyd, Mnadhimu wa jeshi la Marekani, Jenerali Mark Milley, aliiambia Kamati ya Ulinzi ya Bunge kwamba hakuna “ushahidi kamili unaothibitisha viashiria vya ubaguzi wa rangi au upendeleo" katika jeshi la Marekani.

Mke wa Rick, Cynthia anaiambia TRT Afrika kwamba Waafrika wengi wanaotamani kuhama wanaonekana kutofahamu hali halisi ya Marekani. "Utataka tu kwenda kule huku ukifikiria utapata kile unachokiona kwenye televisheni. Ule ni uongo tu unaoonyeshwa kuhusu Marekani."

Mumewe anathibitisha hili, akisema kwamba wahamiaji wanapofika Marekani, kwa kawaida hutambua "siyo kila kitu king’aacho ni dhahabu".

Wanandoa hao wanasema simulizi lao linaakisi maisha ya Wamarekani weusi wengi wanaokumbwa na ubaguzi wa rangi nchini Marekani. Kulingana na Rick, hatua yao imewashawishi Waafrika kadhaa kurejea barani humo kutoka Marekani na Ulaya.

"Kuna Wagambia wengi ambao wamerejea baada ya kujionea tofauti kati ya Gambia na Marekani," Rick anasema. "Wengi wao wamerejea kutoka Marekani, Ujerumani, Uingereza na kwingineko kwa sababu hapa ndio kuna matumaini ya siku zijazo."

Kukabiliana na changamoto barani Afrika

Gambia

Akiwa shambani kwake, Rick anasema kwa sasa anachukulia hio sehemu kama"bustani" zaidi kuliko shamba kamili. Anatumai kuikuza na siku moja kulima mazao kwa njia asili (bila pembejeo za kemikali) na kufuga mifugo katika kiwango cha kibiashara zaidi.

Cynthia na Rick wote wanakubali kwamba wanakabiliwa na changamoto nchini Gambia. Kwa kuwa wamekulia Marekani, ambapo miundombinu ni nzuri, moja ya changamoto kuu inayowakabili wanandoa hao ni ukosefu wa usambazaji wa umeme thabiti. Ufisadi pia ni balaa lingine.

"Kama tunaweza tu kupunguza rushwa katika bara hili na kulipa mishahara inayostahili kuishi, huo utakuwa mwanzo mzuri," anasema Rick.

Anaamini hatua hizo litasaidia pakubwa katika kudhibiti wimbi la uhamaji mkubwa kutoka Afrika.

Wakati Marekani kwa ujumla inabakia kuwa na maendeleo zaidi kuliko nchi yoyote ya Afrika, Rick ana furaha kuhusu bara hilo kuwa bora. Anaamini changamoto za sasa "sio mbaya zaidi kuliko kushughulika na mambo huko Merekani".

"Hakuna mahali palipokamilika kwa kila kitu," anasema Rick. "Ni bora zaidi kuwekeza hisa katika sehemu inakuwa, kuliko mahali panapodidimia”. Ukweli ni kwamba Afrika inatia matumaini kwa siku zijazo."

TRT Afrika