Zaidi ya malori kumi kutoka mashirika ya misaada yamevuka na kuingia nchini Sudan kutoka kwenye mpaka wa Adre na Chad, ikiwa imesheheni misaada kwa ajili ya watu wa eneo la Darfur wanaokabiliwa na baa la njaa, Umoja wa Mataifa umesema.
" Malori ya chakula iliyolenga jamii zilizokata tamaa katika eneo la Darfur imevuka mpaka wa Adré kutoka Chad, baada ya kuzuiwa kwa miezi sita,"Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limesema.
" Malori yetu sasa yanaelekea Darfur kupeleka chakula kuokoa maisha ya watu walio na mahitaji muhimu," limesema Shirika hilo.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limepongeza hatua hiyo, likisema misaada muhimu itakayotolewa itasaidia zaidi ya watu 12,000 wanaohitaji msaada.
"WFP inasema lori hizo zilikuwa zimebeba mtama, kunde, mafuta, na mchele ambao utawanufaisha takriban watu 13,000 ambao wako katika hatari ya njaa katika eneo la Kereneik huko Darfur Magharibi," msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric aliwaambia waandishi wa habari huko New York, Jumatano.
Wiki iliyopita, baraza kuu la Sudan lilisema kuwa litaruhusu matumizi ya kivuko cha mpaka cha Adre na Chad kwa muda wa miezi mitatu-hatua iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na mashirika ya misaada.
Wachunguzi wa kimataifa wanasema kuwa zaidi ya watu milioni 6 wanakabiliwa na uhaba wa chakula katika eneo la Darfur, ambalo linadhibitiwa zaidi na vikosi vya RSF
"Kufunguliwa upya kwa kivuko cha Adre ni hatua muhimu katika juhudi za kuzuia njaa kuenea kote Sudan, na lazima sasa kiendelee kutumika. Nataka kushukuru pande zote kwa kuchukua hatua hii muhimu kusaidia WFP kupata msaada wa kuokoa maisha kwa mamilioni ya watu walio katika uhitaji mkubwa,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Cindy McCain.
Kulingana na WFP, kivuko cha Adre kutoka Chad ndiyo njia fupi na rahisi zaidi katika kufikisha misaada ya kibinadamu nchini Sudan, hasa katika eneo la Darfur, kwa kiwango na kasi inayohitajika kukabiliana na janga kubwa la njaa.
Kutoka Adre, malori yanaweza kuvuka hadi Darfur na kufikia sehemu muhimu za usambazaji siku hiyo hiyo.