Ufaransa, Uingereza na Marekani zinaunga mkono MINUSUMA kuendelea kusalia nchini Mali  / Picha : AFP/ MICHELE CATTANI

Serikali ya Mali imeutaka Umoja wa Mataifa (UN) kuondoa kikosi chake cha kulinda amani nchini humo, MINUSMA.

Waziri wa mambo ya nje Abdoulaye Diop alisema Ijumaa kwamba operesheni "imeshindwa" kufikia lengo lililokusudiwa, akiomba wanajeshi kujiondoa kutoka kwa taifa "mara moja.''

"Serikali ya Mali inatoa wito wa kujiondoa bila kuchelewa kwa MINUSMA," alisema Diop.

Katika mkutano wake Ijumaa, baraza la amani na usalama la Umoja huo lilijadili pendekezo la ujumbe wake nchini Mali kuongezewa muda baada ya awamu yake kwisha 30 Juni.

Diop aliiambia baraza hilo kuwa MINUSMA "haiwezi kukabiliana na changamoto za usalama za Mali."

"MINUSMA inaonekana kuwa sehemu ya tatizo kwa mivutano ya kijamii inayohatarisha amani , maridhiano na kudhoofisha mshikamano wa kitaifa nchini Mali," alisema Diop.

Ukosefu wa imani

Lakini Umoja wa Mataifa unasema vikosi vyake vya MINUSMA vimechangia vikubwa kwa amani nchini humo.

El-Ghassim Wane, mkuu wa Ujumbe wa kikosi cha Mali (MINUSMA) alisema kikosi hicho kimekuwa cha manufaa.

"Licha ya mazingira magumu ambayo MINUSMA inaendesha shughuli zake na vikwazo vingi vinavyokabiliana navyo - ikiwa ni pamoja na vikwazo vya uhuru wa kutembea - MINUSMA imejitahidi kutekeleza mamlaka yake kwa njia bora zaidi," Wane alisema.

Kufuatia kuongezeka kwa uasi 2012, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usalama nchini Mali (MINUSUMA), ulianzishwa na baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Aprili 2013 ili kuleta utulivu nchini humo.

Mnamo Juni 2014, Baraza la Usalama liliazimia kwamba ujumbe huo uzingatie majukumu mengine kama vile ulinzi wa raia, kutetea haki za binadamu, kusaidia maridhiano na kusaidia kurejesha utawala kwa serikali ya raia.

Jumla ya wafanyakazi 17,430 wa Umoja wa Mataifa wakiwemo wanajeshi 11,739 wametumwa nchini Mali kwa ajili ya kulinda amani.

Nchi kadhaa zikiwemo Ufaransa, Uingereza na Marekani zinaunga mkono MINUSUMA kuendelea kusalia nchini Mali.

Mwakilishi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Nicolas de Riviere, alisema ujumbe wa MINUSUMA nchini Mali ni "kwa ajili ya utulivu wa eneo zima".

TRT Afrika