Mkataba uliotiwa saini siku ya Jumatatu na pande mbili zinazopigana - jeshi la Sudan na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces - unaolenga kupata njia salama ya misaada ya kibinadamu na kusisitiza mazungumzo mapana zaidi yanayofadhiliwa na Marekani na Saudi Arabia.
Siku ya Jumamosi, walioshuhudia walisema kuwa Khartoum ilikuwa shwari, ingawa mapigano ya hapa na pale yaliripotiwa usiku kucha. Shirika la utangazaji la Ghuba la Al-Arabiya liliripoti baadhi ya mapigano kaskazini Magharibi mwa Khartoum na kusini mwa Omdurman, mji jirani na mji mkuu.
Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, Rapid Support Forces, RSF, ilishutumu jeshi kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na kuharibu maeneo ya nchi hiyo katika shambulio la anga. Jeshi lilikuwa limeshutumu RSF siku ya Ijumaa kwa kulenga sehemu yakutengeneza sarafu.
Jeshi lilisema wakati huo huo wito wake wa Ijumaa kwa askari wa akiba ni uhamasishaji wa sehemu na hatua ya kikatiba, na kuongeza jeshi linatarajia idadi kubwa kuitikia wito huo.
Mzozo huo uliozuka Aprili 15, umesababisha vifo vya takriban raia 730 na kusababisha Wasudan milioni 1.3 kuondoka makwao, wakikimbia nje ya nchi au katika maeneo salama ya nchi.
Wale waliosalia Khartoum wanatatizika kwa kukosa huduma kama vile umeme, maji na mitandao ya simu. Waporaji wamepora nyumba, haswa katika vitongoji vilivyo na wakazi wenye uwezo wa maisha.
Siku ya Jumamosi, polisi wa Sudan walisema walikuwa wakiongeza jitihada na pia kuwaita maafisa waliostaafu wenye uwezo kusaidia.
"Kitongoji chetu kimekuwa eneo la vita. Huduma zimeporomoka na machafuko yameenea Khartoum," Ahmed Salih mwenye umri wa miaka 52, mkazi wa jiji hilo alisema.
"Hakuna anayesumbuka kuwasaidia watu wa Sudan, si serikali wala nchi za kimataifa. Sisi ni binadamu, ubinadamu uko wapi?" aliongeza.
Mashirika ya misaada yanasema kuwa licha ya mapatano hayo yametatizika kupata dhamana ya ukiritimba na usalama wa kusafirisha misaada na wafanyakazi katika maeneo salama ya nchi hadi Khartoum na maeneo mengine yenye joto. Maghala pia yameporwa.
Mapigano pia yameenea katika eneo dhaifu la Darfur, na kuathiri zaidi mji wa magharibi wa El Geneina, ambao umeshuhudia mashambulizi ya wanamgambo ambayo yameharibu miundombinu yake na kuua mamia.