Vikosi vya usalama vya Somalia vinasema operesheni za hivi karibuni zimetoa pigo kubwa kwa al-Shabaab. Picha: AP

Magaidi 70 wa al-Shabaab wameuawa katika operesheni iliyofanywa na Jeshi la Taifa la Somalia katika mkoa wa Mudug.

Majeshi ya usalama yakisaidiwa na vikundi vya vijana wa eneo hilo, walivamia maficho na sehemu za mkusanyiko wa magaidi wa al-Shabaab katika mji wa Aad.

Viongozi waandamizi wa kundi hilo la kigaidi walikuwa miongoni mwa wale waliouawa katika operesheni hiyo, kulingana na Naibu Waziri wa Habari wa Somalia, Abdirahman Yusuf Al Adala, aliyeeleza kwenye vyombo vya habari vya eneo hilo.

Wizara ya Ulinzi ya Somalia, ambayo pia ilitangaza kuhusu operesheni hiyo Jumapili, ilisema "hatua za kijeshi za hivi karibuni katika Mudug na Galgaduud zimekuwa pigo kubwa kwa Khawarij na makundi yao ya wanamgambo."

Khawarij ni neno ambalo serikali ya Somalia hutumia kuelezea kundi la kigaidi la al-Qaeda lijulikanalo kama al-Shabaab.

Operesheni hiyo inakuja siku moja baada ya milipuko ya bomu la lori kwenye kizuizi cha jeshi katika mji wa kati wa Beledweyne na kuua zaidi ya watu 18, wakiwemo wafanyakazi 10 wa usalama, na kujeruhi wengine zaidi ya 40.

Jumamosi, shambulio la angani katika mji wa Elbur unaodhibitiwa na al-Shabaab lililenga nyumba ya mkutano na kuua viongozi waandamizi wa al-Shabaab, kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Somalia.

AA