Wakuu wa Majeshi ya Anga kutoka nchi 40 barani Afrika wanakutana jijini Lusaka Zambia kujadiliana namna ya kushirikiana katika utoaji wa misaada wakati wa majanga.
Akihutubia mkutano wa 14 wa wakuu hao (AAAC), Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amebainisha kuwa majanga hayachagui mipaka wala itikadi, na kusisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuendelea kushirikiana bila kujali umbali nchi na nchi.
"Zambia ilikumbwa na ukame mkubwa ambao umesababisha baadhi ya jamii kukimbia makazi yao. Hili ni jambo la kawaida kabisa kutokea barani Afrika na kudhihirisha haja na haraka ya kushirikiana kati ya nchi zetu hususani katika ngazi ya majeshi ya anga," alisema Hichilema katika risala yake iliyosomwa na Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Zambia Douglas Syakalima.
Kamanda wa Jeshi la Anga nchini Zambia, Oscar Nyoni, alisema mkutano huo unalenga kukuza na kuimarisha ushirikiano wa majeshi hayo.