Matumaini ya amani Sudan yaongezeka baada ya Mkuu wa Jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan, na Kamanda wa kikosi cha RSF Mohammed Hamdan Dagalo maarufu Hemedti kukubali kufanya kikao cha kihistoria kumaliza machafuko Sudan, afisa wa ngazi ya juu wa Sudan amefichua kulingana na jarida la Sudan Tribune.
Tangu Aprili 15, 2023, machafuko yamezuka nchini humo kati ya mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al Burhan na naibu wake wa zamani, ambaye sasa ni kamanda wa Kikosi cha RSF Mohamed Hamdan Daglo.
Mkutano kati ya Abdel Fattah al-Burhan, mwenyekiti wa Baraza Kuu na Kamanda Mkuu wa Jeshi La Sudan, kufichua mipango ya kufanya mazungumzo na Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama" Hemetti," Kamanda wa Kikosi cha msaada wa haraka (RSF) haujulikani utafanyika lini.
Taarifa hiyo inafuatia matamshi ya Jeneral Al-Burhan akiwahutubia wanajeshi wa Sudan katika eneo la kijeshi la Bahari Nyekundu siku chache tu zilizopita ambapo alidokeza uwezekano wa kujadiliana na kikosi cha wapiganaji cha RSF.
Mkutano kati ya wawili hao unatarajiwa kufanyika katika siku zijazo na kuwa na ushawishi mkubwa kwenye mzozo unaoendelea nchini humo.
Mnamo Desemba 9, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Pemebezoni mwa Afrika, IGAD ilifanya mkutano wa kilele ambapo ilitangazwa kuwa majenerali hao wawili wangesaini makubaliano ya kusitisha mapigano na kurudi kwenye meza ya mazungumzo.
IGAD ilishauri kufanyika kwa mkutano kati ya majenerali hao wawili, lakini Burhan anadaiwa kukataa.
Jenerali Burhan ameripotiwa kukataa mkutano huo kwa kusisitiza kuwa ni lazima vikosi vya RSF viondoke kwenye maeneo ya raia kabla ya mkutano huo uliopendekezwa na Hemedti.
Mkutano huo wa IGAD kuhusu Sudan ni mojawapo ya juhudi mbalimbali za kidiplomasia zilizoendeshwa ikiwemo pamoja na Umoja wa Afrika AU, Saudi Arabia na washirika wengine wa kimataifa ili kufanikisha utekelezaji wa upatanishi.