Sudan ipo ukingoni mwa 'vita vya wenyewe kwa wenyewe': Mjumbe wa UN Sudan asema akijiuzulu

Sudan ipo ukingoni mwa 'vita vya wenyewe kwa wenyewe': Mjumbe wa UN Sudan asema akijiuzulu

Takriban watu 5,000 wameuawa na zaidi ya 12,000 wamejeruhiwa tangu mzozo kati ya majenerali wapinzani kuanza mwezi Aprili.
Mjumbe wa UN nchini Sudan Volker Perthes akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Khartoum / Picha: Reuters

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes ambaye alikuwa akifanya kazi yake nje ya Sudan, baada ya kupigwa marufuku kuingia Sudan na uongozi wa kijeshi wa nchi hiyo, ametangaza kujiuzulu huku akionya kuwa mzozo kati ya viongozi wa pande za kijeshi Sudan "unaweza kugeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe".

Akitoa hotuba yake ya mwisho kwa Baraza la Usalama, Volker Perthes, alisema kuwa mapigano hayo hayaonyeshi dalili ya kutamatika, na hakuna upande unaokaribia "ushindi wa kijeshi wa kuamua." Ameongeza kuwa vurugu vya eneo la Magharibi la Darfur nchini Sudan "zimezidi kuwa mbaya zaidi", huku raia wakilengwa kwa mujibu wa kabila lao.

Uhasama kati ya jeshi la Sudan, linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan, na Vikosi vya RSF, vinavyosimamiwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, vilianza mapigano ya wazi katikati ya Aprili.

Takriban watu 5,000 wameuawa na zaidi ya 12,000 kujeruhiwa tangu mzozo kati ya majenerali wapinzani kuanza mwezi Aprili. Perthes alisema kwamba idadi halisi "ni kubwa zaidi.”

Mjumbe Perthes alisema kuwa kulikuwa na angalau makaburi 13 ya halaiki ndani na karibu na Geneina, mji mkuu wa Mkoa wa Darfur Magharibi, kwa mujibu wa ripoti za kuaminika zilizopokewa na Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu ya UN.

Makaburi hayo yalitokana na mashambulizi ya RSF na wanamgambo washirika wao dhidi ya raia, wengi wao wakiwa watu weusi kutoka jamii za kiafrika, Perthes alisema.

Eneo la Magharibi la Darfur lilikuwa eneo lililokabiliwa na mauaji ya kimbari mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Wakati huo huo mkurugenzi wa shughuli za ofisi ya kibinadamu ya UN, Edem Wosornu, aliliambia baraza hilo kuwa zaidi ya watu milioni 20 ambao ni takriban nusu ya idadi ya raia wa Sudan wanakabiliwa na njaa kali na ukosefu wa usalama wa chakula.

"Zaidi ya watu milioni 6 sasa wako hatarini kutokana na njaa," alisema. "Ikiwa mapigano yataendelea, uwezekano wa hili kuwa janga kubwa linakaribia kuwa ukweli kila siku.”

Mapigano hayo yamewapelekea watu milioni 4.1 kukimbilia maeneo mengine salama nchini Sudan huku zaidi ya milioni 1 wakisaka hifadhi katika nchi jirani, Wosornu alisema, huku akisisitiza kuwa uhamishaji na ukosefu wa usalama "umesababisha visa vya unyanyasaji wa kijinsia kwa viwango vya kuogofya.”

Perthes, alikuwa muhimu wa upatanishi baada ya mzozo kuibuka, lakini serikali ya kijeshi ilidai alikuwa na upendeleo na kumfahamisha Katibu mkuu wa UN Antonio Guterres mnamo Juni 8 ya kwamba haruhusiwi nchini Sudan.

Mfanyakazi wetu hawezi kutangazwa kuwa mtu asiyekubalika na serikali kwani hilo linakwenda kinyume na mkataba wa UMOJA wa Mataifa

Antonio Guterres, UN

Kwa upande wake, Perthes, ambaye amekuwa mwakilishi maalum wa Sudan tangu alipoteuliwa mnamo Januari 2021, aliwashauri pande zinazopigana kumaliza mgogoro wao na kuwaonya kuwa "madhambi yao yataadhibiwa.” Aliyasema hayo akitangaza kujiuzulu kwake.

"Kutakuwa na uwajibikaji kwa madhambi yote," alisema.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema kwenye mkutano wa waandishi wa habari ya kwamba alikubali ombi la kujiuzulu kwa Perthes, kwani "ametoa sababu za kuaminika za kujiuzulu.” bila kutoa ufafanuzi zaidi.

AP