Haijawahi kuingia akilini mwa Ezz El-Din Dahab kwamba katika karne hii ya 21 atatumia barua zilizoandikwa kwa mkono kuwasiliana na jamaa zake huko Sudan.
"Barua zilizoandikwa kwa mkono ndio njia pekee inayopatikana ya mawasiliano wakati wa vita vinavyoendelea sasa nchini Sudan," Dahab anasema.
Ghasia nchini Sudan zilianza tangu mwezi Aprili mwaka huu, huku kukiwa na mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na kundi la Rapid Support Forces (RSF).
Vurugu hizo zimetatiza kabisa huduma za simu na mtandao katika maeneo kadhaa nchini, na kuwaacha wakazi bila njia nyingine ila kutumia barua zilizoandikwa kwa mkono kama mawasiliano.
Katikati ya ghasia hizo, wananchi wa Sudan sasa wanatumia madereva wa mabasi kama posta kusafirisha barua zao kwa familia katika miji mingine.
"Vita vimegharimu maelfu ya maisha ya watu nchini Sudan," Dahab alisema.
Tangu kuzuka kwa ghasia nchini Sudan, maelfu wameuawa na zaidi ya milioni saba kuhama makazi yao, hasa katika jimbo la Khartoum na Darfur, hayo ni kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.
Mikataba kadhaa ya kusitisha mapigano iliyosimamiwa na wapatanishi kutoka Saudi Arabia na Marekani kati ya mahasimu hao wanaozozana imeshindwa kumaliza uhasama uliopo.
Kukata tamaa
Dahab alisema mitandao ya mawasiliano nchini Sudan, hasa eneo la magharibi mwa Darfur haifanyi kazi.
"Maeneo kadhaa ya Darfur hayatumii mitandao ya mawasiliano," alisema. "Kutumia barua zilizoandikwa kwa mkono kwa mawasiliano si jambo la kushangaza kwa mtu yeyote katika hali ya sasa," aliongeza.
Mwezi uliopita, Umoja wa Mataifa ulisema watu 60 waliuawa na karibu 50,000 walikimbia makazi yao kutokana na mapigano kati ya jeshi na RSF katika mji wa Nyala, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini.
Kulingana na Shirika hilo la Kimataifa, miundombinu ya umeme na maji haifanyi kazi vizuri mjini humo kutokana na athari za vita.
Wakati mapigano yakiendelea, mawasiliano yamekuwa magumu zaidi, hasa katika Darfur, eneo linalokaliwa na takriban robo ya wakazi milioni 48 wa Sudan.
Wakati mgumu
Kwa kawaida wananchi hufika katika ofisi za usafiri kati ya miji mikubwa ili kukabidhi barua zao zilizoandikwa kwa mkono ili kufikwa na madereva wanaosafiri kutoka mji mmoja hadi mwengine.
Amna Musa, 36, mkazi katika mji wa El Geneina, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Magharibi, pia alilazimika kutuma barua ili kuijulia hali familia yake katika jiji la Nyala.
"Tangu huduma ya mtandao iliposimama, nililazimika kuwasiliana na familia yangu huko Nyala kupitia barua zilizoandikwa kwa mkono," Musa alimwambia Anadolu.
Jiji la Nyala ni miongoni mwa maeneo yaliyoathariwa zaidi na vita hasa baada ya kusambuliwa kwa bomu hivyo kuharibu miundombinu yote ya mawasiliano, hayo ni kwa mujibu wa Musa.
"Hatukuweza kupata habari kutoka kwa wapendwa wetu mjini," Musa alisema. "Hizo zilikuwa nyakati za kutisha," aliongeza. "Nilituma barua iliyoandikwa kwa mkono katika siku chache zilizopita kwa familia yangu, na ninasubiri jibu," Musa alisema.
"Kwa hali ya sasa, hatukupata chaguo bora zaidi kwa mawasiliano," aliongeza.
Adam Abdullah, mmiliki wa ofisi ya mabasi ya usafiri, alisema watu wanatumia barua ili kuangalia jamaa zao, "tangu vurugu zilipoathiri nyaya za mtandao."
"Tunapeleka barua zinapokwenda na kurudisha majibu wa wahusika kwa malipo," aliongeza.
Hata hivyo, changamoto kubwa iliyopo kwa watumiaji wa huduma hii, ni jinsi huduma hii inavyokawia kwa walengwa kupata majibu kwa wakati.