Uamuzi wa mahakama ya Rwanda umeidhinisha marufuku ya uchaguzi kwa mwanasiasa wa upinzani Victoire Ingabire, mpinzani mkuu wa Rais Paul Kagame katika uchaguzi ujao nchini humo.
Mahakama imefanya uamuzi ambao umekataa kuondoa masharti ambayo mahakama ilikuwa imemuwekea mwaka 2018.
"Uamuzi huu wa mahakama unakuja wakati ambapo Rwanda inapanga uchaguzi wa bunge na urais, Julai 2024, uchaguzi ambao nilikuwa ninatarajia kugombea nikipigania demokrasia na mabadiliko," Ingabire alisema katika taarifa .
Ingabire amerudi Rwanda kutoka Uholanzi alipokuwa uhamishoni mwaka 2010, akiwa na mpango wa kugombea urais.
Lakini mwaka 2012 kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha FDU-Inkingi, alihukumiwa kifungo cha miaka 15 kwa madai ya "kukana mauaji ya kimbari" na kula njama dhidi ya serikali. Hata hivyo, alikana mashtaka hayo.
Mwaka 2018 aliachiliwa baada ya Rais Paul Kagame kutumia mamlaka yake kutoa msamaha kwa wafungwa.
Msamaha huu ulikuja na masharti mawili. Kwanza ilikuwa ni lazima aombe ruhusa kutoka kwa Waziri wa Sheria kila mara iwapo atataka kutoka nje ya Rwanda. Pili alihitajika kufika mbele ya afisa ya mahakama mara moja kila mwezi.
Masharti haya yanamzuia pia kugombea kiti chochote cha siasa.
Mwaka wa 2023 Ingabire aliwasilisha kesi katika mahakama kuu ya nchi hiyo akiomba masharti haya kuondolewa.
Kesi yake ilisikizwa Februari 2024 na uamuzi umefanyika leo 3 Machi 2024.
Mahakama kuu imekataa kuondoa masharti hayo.
Rais wa Rwanda Paul Kagame amechaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa chama tawala cha Rwanda Patriotic Front.
Atagombea kuhudumu kwa muhula mwingine wa miaka mitano katika nafasi hiyo.