Rais Andry Rajoelina  ajiuzulu kabla ya uchaguzi / Picha: AFP

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina amejiuzulu kutoka madaraka baada ya kuthibitishwa rasmi kama mgombea kwenye uchaguzi ujao wa urais nchini humo uliopangwa kufanyika Novemba 9, vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti siku yaJjumapili.

Rais Rajoelina atakuwa anawania kiti cha rais akiwa ni kati ya wagombea 13 waliothibitishwa na Mahakama ya Juu ya katiba mwishoni mwa wiki huku wengine wakiwa ni marais wawili wa zamani Eric Marc Ravalomanana na Hery Rajaonarimampianina.

"Rajoelina alitii matakwa ya kikatiba na kuwasilisha barua ya kujiuzulu kwake kwa Mahakama kuu ya Kikatiba jumamosi, Septemba 9, " Shirika la habari la ACTU iliripoti, ikinukuu taarifa ya mahakama.

Kulingana na katiba ya Madagascar, rais anayeshikilia madarakani kwa sasa anahitajika kujiuzulu kwanza ikiwa anataka kutafuta kuchaguliwa tena.

Baada ya kujiuzu kwa rais, Mkuu wa Seneti Herimanana Razafimahefa anatakiwa kuchukua madaraka kwa mujibu wa katiba hata hivyo, kwa sasa, Razafimahefa ameripotiwa kukataa, huku akieleza sababu za kibinafsi.

Mahakama kuu ya Katiba ilisema kuwa mamlaka ya rais sasa yatatekelezwa na serikali kwa pamoja na Waziri Mkuu Christian Ntsay kama mkuu, kulingana na ripoti hiyo.

Wapiga Kura nchini Madagascar watapiga kura kwa raundi ya kwanza ya uchaguzi wa rais tarehe 9 Novemba, na ikiwa hakuna mshindi, raundi ya pili ya uchaguzi itafanyika tarehe 20 Desemba.

Kampeni za uchaguzi wa urais zitaanza rasmi Oktoba 10 na kuendelea hadi Novemba 8, kwa mujibu wa tume huru ya taifa ya uchaguzi, huku zaidi ya wapiga kura milioni 10.7 wakitarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo.

Rajoelina, mwenye miaka 49, alishinda kura ya mwisho ya uchaguzi uliopita mnamo desemba 2018 baada ya kumshinda Ravalomanana katika raundi ya pili ya uchaguzi, ambayo ilisemekana kuwa imeharibiwa na makosa.

Awali, kulikuwa na uvumi kwamba mgombeaji Rajoelina angekatazwa kuwania kutokana na utata juu ya kuchukua uraia wa Ufaransa mnamo 2014. Hata hivyo, Mahakama kuu ya Katiba ilisema kuwa, baada ya uchunguzi, ilihitimishwa kuwa hakuna mgombea yeyote, pamoja na Rajoelina, aliyepoteza uraia wake wa Madagascar.

AA