Vijana 28 waendesha baiskeli kutoka Afrika Mashariki wameamua kuzunguka nchi kadhaa kwa kutumia usafiri wa baiskeli kwa lengo la kuhamasisha usalama wa chakula / Picha : TRT Afrika 

Ajenda ya tabia nchi imezidi kushika kasi. Viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa wamekuwa wakikutana katika majukwaa mbalimbali kujadiliana na kutafuta suluhu ya pamoja ya kuweza kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ambayo athari zake zinaelezwa kuwa tishio kwa dunia.

Mkutano wa hivi karibuni, ni ule uliofanyika jijini Nairobi nchini Kenya, ambapo viongozi kutoka nchi mbalimbali za bara la Afrika walikutana na kutoa maoni yao.

Wakati hayo yakijiri, vijana wa rika mbalimbali kutoka mataifa saba ya Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na DRC wameamua kuunganisha nguvu na kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi kwa namna tofauti.

Vijana hawa 28 ambao wote ni waendesha baiskeli wameamua kufanya ziara ya eneo la Afrika Mashariki kwa kutumia usafiri wa baiskeli.

''Lengo kuu ni kujenga uelewa kuhusu mchakato wa mtangamano wa EAC,'' anasema Muasisi wa mradi, John Bosco Balongo. ''Kila mwaka kuna mada tofauti juu ya mtangamano wa EAC, hivyo mwaka huu, kaulimbiu imekuwa ni Mabadiliko ya Tabia Nchi na usalama wa chakula,'' anasema Balongo.

''Hiki ni mojawapo ya vituo vingi ambavyo tumekuwa navyo tangu tuanze ziara yetu ya baiskeli tarehe 1 mwezi Agosti. Tumekuwa tukipitia Afrika Mashariki. Tulianzia Uganda, ikaenda Kenya, Tanzania, Burundi na Rwanda sasa Uganda inakwenda kukamilisha.'' Balongo anaelezea TRT Afrika.

Changamoto zilizowakumba

''Tulichagua kutumia baiskeli kutoa ufahamu kuhusu mchakato wa ushirikiano wa EAC kwa sababu unaashiria uendelevu na kukuza mtindo wa maisha wenye afya,'' aliendelea kusema Balongo. ''Zaidi ya hayo, uendeshaji wa baiskeli huturuhusu kufikia hadhira pana zaidi kwa kuwa tunaweza kushughulikia maeneo mengi zaidi na kushirikiana na watu katika jumuiya tofauti.''

Lakini bila shaka kumekuwa na changamoto hasa kuhusiana na usafiri kutoka nchi moja hadi nyingine

“Lugha, malori makubwa njiani, kuharibika kwa baiskeli, uchafu wa maji katika baadhi ya maeneo, fedha kidogo, baridi, mawasiliano kwani inatubidi kununua sim kadi 7 unapovuka mipaka 7 ya washirika wa EAC, na nyingi,” anaelezea Balongo

Hafla hiyo ilileta pamoja kundi la watu mbalimbali, huku Mkurugenzi wa Michezo na Utamaduni wa Vijana kutoka Burundi akieleza nia yake ya kuandaa hafla hiyo mwakani.

TRT Afrika