Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed and mkewe Zinash Tayachew wamevumbua kampeni ya kupanda miche milioni 500 kwa siku moja / Picha EthiopiaPMO

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amezindua kampeni kubwa ya upandaji miti siku ya Jumatatu.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed na mkewe Zinash Tayachew walizindua rasmi mpango huo uitwao Green Legacy katika mji mkuu Addis Ababa wakianza na kupanda miche ya tufaha.

Wananchi wanatarajiwa kuiga mfano huo na mwisho wa siku mamlaka inatumai miti milioni 500 itapandwa. Ofisi ya Waziri Mkuu imesambaza picha za uzinduzi huo na watu wanaoishi na ulemavu wakishiriki.

Ethiopia inalenga kuvunja rekodi yake ya kupanda idadi kubwa zaidi ya miti kwa siku kama sehemu ya kampeni yake ya kukabiliana na athari za ukataji miti na mabadiliko ya hali ya hewa.

Rekodi ya dunia

Ethiopia ilijiwekea rekodi mnamo Julai 2019 kwa kupanda miti milioni 353 kwa saa 12 tu, kulingana na maafisa, na inatarajia kuvuka alama Jumatatu. "Lengo letu ni kuvunja rekodi yetu!" Waziri Mkuu Abiy Ahmed alitweet.

“Mashindano yetu ni sisi wenyewe, tunaamini mikoa, kanda, wilaya na vijiji vitavunja rekodi zao wenyewe kwa kupanda zaidi ya mwaka jana, kila mmoja wetu avunje rekodi zake,” aliongeza.

Guinness World Records bado haijathibitisha rekodi hiyo na Ethiopia.

Rekodi ya sasa ya dunia ya miti iliyopandwa kwa siku moja inashikiliwa na India baada ya zaidi ya watu 800,000 kupanda miti milioni 50 mwaka 2016 katika jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh.

Kampeni ya Ethiopia inalenga kurejesha misitu ya nchi hiyo ambayo imepungua kutoka 35% ya ardhi yote mwishoni mwa karne ya 19 hadi karibu 4% katika miaka ya 2000, kulingana na Umoja wa mataifa.

TRT Afrika