Na Omar Abdel-Razek
Kuendelea kuongezeka kwa shughuli za kijeshi katika Bahari Nyekundu kunaleta madhara makubwa ya kiuchumi, usalama na mazingira ya bara la Afrika.
Ingawa ni nchi chache za Kiafrika zinafaidika na uwepo wa bahari hiyo, bado nyingi zitabeba mzigo mkubwa wa uharibifu wa mazingira na mfumuko wa bei.
Kati ya nchi nane zinazopatikana Bahari Nyekundu, tano ni za Kiafrika. Hata hivyo, vyombo vya habari bado vinaendelea kupuuzia hasara inayotokana na shughuli hizo.
Badala yake, ufuatiliaji mkubwa wa suala hili umewekwa kwenye athari za kiuchumi zinazoweza kutokea kwa watumiaji wa Magharibi kutokana na usumbufu wa usafirishaji katika moja ya njia za maji zenye shughuli nyingi zaidi duniani.
Mgogoro huo ulianza Novemba wakati kundi la Houthis kutoka Yemen kuanza kulenga meli kubwa na meli za mizigo zinazopitia mlango wa bahari wa Bab-al-Mandab wenye upana wa kilomita 32 katika kukabiliana na mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, yanayoendelea kwa sasa.
Mamia ya meli za mizigo na mafuta zililazimika kuzunguka Afrika, na kuongeza siku 12 zaidi na kilomita 6000 kwa safari zao kwa wastani.
Hili limeongeza bei za mafuta na gharama za bima, ambayo bila shaka ni mzigo mkubwa kwa watumiaji na itaathiri uchumi wa dunia.
Takribani asilimia 15 ya biashara duniani, yenye thamani ya dola trilioni 1 hupitia Bahari Nyekundu, na kupitia mfereji wa Suez, nchini Misri.
Suala hili linaufanya msimamo wa Misri katikati ya mgogoro huu kuwa mgumu, ikizingatiwa kuwa biashara ya Bahari Nyekundu ni chanzo kikuu cha mapato ya taifa.
Mapato kutoka mfereji wa Suez yalichangia zaidi ya dola bilioni 10 kwenye uchumi wa Misri, kwa mwaka 2023 pekee.
Hata hivyo, kulingana na taarifa kutoka Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD), kumekuwa na anguko la mapato kwa asilimia 42 katika miezi miwili iliyopita, muenendo ambao utakuwa na athari kubwa iwapi shughuli za kijeshi zitaendelea.
Muda haungeweza kuwa muhimu zaidi kwa Misri, nchi yenye watu wengi zaidi katika Mashariki ya Kati na mojawapo ya nchi zenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika.
Uchumi wa Misri unakabiliana na uhaba mkubwa wa fedha muhimu kwa ajili ya kulipia uagizwaji mkubwa wa bidhaa na kuongezeka kwa madeni ya nje ambayo yamezidi dola bilioni 160.
Usalama Bahari Nyekundu
Lakini mtanziko wa Misri katika muktadha huu unaenea zaidi ya masuala ya kiuchumi.
Kihistoria, Bahari Nyekundu imekuwa na umuhimu mkubwa wa kimkakati kwa usalama wa Misri kuanzia enzi ya Malkia Hatshepsut, alipotuma msafara muhimu wa kibiashara katika ardhi ya Punt(Somalia ya sasa) kati ya 1479-1458.
Wakati wa Vita vya Oktoba mwaka wa 1973, Misri ilizuia mlango wa bahari wa Bab al-Mandab ili kuzuia usambazaji wa kijeshi kwa Israeli.
Hata hivyo, Cairo kwa sasa inajiepusha kuidhinisha hatua za kijeshi za Magharibi dhidi ya Houthis, yaani Operesheni inayoongozwa na Marekani ya 'Walezi wa Ufanisi', ili kuepuka kuonekana kutojali chanzo cha mzozo huo—Vita dhidi ya Gaza.
Nchi nyingine za Bahari Nyekundu za Afrika zinakabiliwa na changamoto zao. Sudan inakabiliana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, wakati Somalia inakabiliana na mgogoro wake wa hivi majuzi na Ethiopia kufuatia nchi hiyo kusaini mkataba na Somaliland iliyojitenga.
Makubaliano hayo yanaipa Ethiopia haki ya ukodishaji wa miaka 50 kwa kilomita 20 za ukanda wa pwani, badala ya kutambuliwa rasmi kwa uhuru wa Somaliland.
Jitihada hizo za Ethiopia zimekumbana na upinzani kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Misri, Eritrea na Saudi Arabia, jambo ambalo limekuwa likitatiza usalama wa Bahari Nyekundu.
Hali ya sasa na athari zake inasisitiza kutokuwepo kwa nchi za Afrika zinazopakana na Bahari Nyekundu kutoka kwa mipango yoyote ya usalama wa baharini kuhusu njia hii muhimu ya maji.
Kwa takriban miongo mitatu, usalama wa Bahari Nyekundu umekuwa nje ya udhibiti wa mataifa yake ya Kiafrika (Misri, Sudan, Somalia, Eritrea, na Djibouti), na kusababisha nchi nyingi kugombea udhibiti wa bandari zake kwa madhumuni ya kijeshi na kibiashara.
Mgogoro wa sasa unaweza kuzidisha hali hii, kwa kutarajia kwamba jumuiya ya kimataifa inaweza kubuni mbinu mpya ya kukabiliana na vitisho vya kijeshi katika Bahari ya Nyekundu, sawa na majibu kufuatia kuibuka kwa uharamia nchini Somalia, uwezekano wa kusababisha kuongezeka kwa uwepo wa kigeni na mifumo ya kisheria katika ukanda huo.
Hasara nyingi kuliko faida
Upangaji upya wa meli kuzunguka Rasi ya Good Hope kunaweza kutoa manufaa ya muda kwa baadhi ya bandari nchini Afrika Kusini, Namibia, na Mauritius, kulingana na kampuni kubwa ya usafirishaji A.P. Moller-Maersk A/S.
Hata hivyo, wataalam wanaonya kwamba mafanikio haya yanaweza kupitiwa na ushuru mpana zaidi ambao Afŕika itakabiliana nao.
Taasisi ya Earnest & Young inatabiri ongezeko la asilimia 0.7% katika mfumuko wa bei duniani kwa mwaka 2024 iwapo usumbufu wa aina hiyo utaendelea, na kuathiri uagizaji wa bidhaa kutoka Afrika na malipo ya madeni.
Mataifa ya Afrika Mashariki, yanategemea sana uagizaji wa nafaka na bidhaa kutoka Umoja wa Ulaya na nchi za Bahari Nyeusi, yanatarajiwa kubeba mzigo mkubwa, huku gharama za mizigo zikiweza kupanda kwa karibu dola 8 kwa tani, kama ilivyobainishwa na Baraza la Kimataifa la Nafaka.
Hasara kwa bara la Afrika kutokana na mzozo wa Bahari Nyekundu zinaweza kuenea zaidi ya ushuru wa kiuchumi na kujumuisha uharibifu wa mazingira.
Hatari ya kumwagika kwa mafuta kutokana na mgomo unaowezekana dhidi ya meli za mafuta wakati wa harakati za kijeshi inaleta tishio kubwa kwa viumbe vya baharini katika eneo hilo.
Mfumo wa ikolojia wa miamba ya Bahari Nyekundu, ambao ni muhimu kwa usalama wa chakula na maisha ya wakazi milioni 28 wa pwani, pia uko hatarini.
Ongezeko la idadi ya meli kubwa na meli za mafuta zinazozunguka Afrika kunahitaji kusimama kwa shughuli za kujaza mafuta.
Hata hivyo, bandari nyingi za Afrika hazina vifaa vya kutosha vya kushughulikia meli kubwa kama hizo na zinakabiliwa na msongamano na vifaa duni, kama ilivyoripotiwa na shirika la habari la Reuters.
Kwa hivyo, hali hii huongeza uwezekano wa ajali kama vile kumwagika kwa mafuta.
Athari za mzozo wa Bahari Nyekundu huenea zaidi ya nchi zilizo karibu na kuathiri bara zima.
Umoja wa Afrika unapaswa kuchukua jitihada za dhati za kidiplomasia ili kupunguza hatari hizi, kwani usalama wa chakula na mazingira wa Afrika haupaswi kuamuliwa na mataifa makubwa na ya kikanda pekee.