Misri imesema itajiunga na kesi ya mauaji ya halaiki iliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuhusu hujuma yake mbaya katika Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa yake Jumapili, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilisema hatua hiyo imekuja "kutokana na ukali na ukubwa wa mashambulizi ya Israel dhidi ya raia wa Palestina huko Gaza na kuwalenga raia na uharibifu wa miundombinu katika ukanda huo."
Zaidi ya Wapalestina 35,000 wameuawa na wengine zaidi ya 76,600 kujeruhiwa katika hujuma ya kikatili ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza tangu shambulio la Hamas Oktoba 7 mwaka jana na kuua karibu watu 1,200.
Miezi saba ya vita, maeneo makubwa ya Gaza yalikuwa magofu huku kukiwa na kizuizi cha chakula, maji safi na dawa.
SA inataka Israel iondoke Rafah
Uamuzi wa muda uliotolewa na mahakama yenye makao yake mjini The Hague mwezi Januari ulisema "inawezekana" kwamba Tel Aviv inafanya mauaji ya halaiki huko Gaza, na kuiamuru kukomesha vitendo hivyo na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba msaada wa kibinadamu unatolewa kwa raia huko Gaza.
Siku ya Ijumaa, Afrika Kusini iliitaka ICJ kuamuru Israel iondoke Rafah kama sehemu ya hatua za ziada za dharura kuhusu vita.