Mamlaka ya bandari imesema matokeo ya uchunguzi wa afya yatajulikana baada ya saa 48./ Picha : Reuters 

Mauritius ilizuia meli ya kampuni ya Norwegian Cruise Line Holdings kutia nanga kwenye bandari zake kutokana na kile ilichosema ni hatari kiafya na kuchukua sampuli kutoka kwa takriban abiria 15 waliokuwa wametengwa ndani ya meli hiyo, mamlaka ya bandari yake ilisema Jumapili.

Meli hiyo ya kitalii ya Norwegian Dawn (NCLH.N), ilikuwa imepangwa kutia nanga huko Port Louis siku ya Jumapili, lakini kwa kuwa haikuwa imeenda kwenye Kisiwa cha Reunion, ilifika Port Louis siku moja mapema, Mamlaka ya Bandari ya Mauritius ilisema katika taarifa.

"Uamuzi wa kutoruhusu meli ya watalii kuingia kwenye kituo hicho ulichukuliwa ili kuepusha hatari zozote za kiafya," mamlaka hiyo ilisema.

Msemaji wa Meli hiyo yenye makao yake makuu Marekani alisema katika taarifa yake kwamba wakati wa safari ya meli hiyo nchini Afrika Kusini mnamo Februari 13, baadhi ya abiria walipata dalili kidogo za ugonjwa unaohusiana na tumbo.

"Afya na usalama wa abiria pamoja na ile ya nchi kwa ujumla ni ya juu kabisa kwa mamlaka,"aliongeza afisa wa Mauritius , bila kutoa maelezo yoyote juu ya asili ya hatari ya kiafya.

Mara baada ya kufika Port Louis, wasimamizi wa meli hiyo walifanya kazi na mamlaka ya Mauritius kuhakikisha kuwa tahadhari zipo na wote waliokuwemo wako sawa, msemaji huyo alisema.

Mamlaka ya bandari imesema matokeo ya uchunguzi wa afya yatajulikana baada ya saa 48.

Meli hiyo ina abiria 2,184 na wafanyakazi 1,026. Kati ya hao, takriban abiria 2,000 wangeshuka Port Louis baada ya kumaliza safari yao huku abiria wengine 2,279 wapya wakitarajiwa kupanda meli, mamlaka ya bandari ilisema.

Reuters