Waziri mkuu aliye madarakani nchini Mauritius, Pravind Jugnauth, alisema Jumatatu kwamba muungano wake wa kisiasa unaelekea kushindwa kufuatia uchaguzi wa bunge uliofanyika Jumapili.
"L'Alliance Lepep inaelekea kushindwa. Nimejaribu kufanya niwezavyo kwa ajili ya nchi na wananchi. Wananchi wameamua kuchagua timu nyingine. Naitakia nchi mafanikio mema," Jugnauth aliwaambia waandishi wa habari.
Wamauritius walipiga kura kuwachagua wabunge 62 kwa miaka mitano ijayo, huku kukiwa na vyama 68 na miungano mitano ya kisiasa.
Vigezo vya kushinda
Chama au muungano wowote unaopata zaidi ya nusu ya viti bungeni pia utashinda wadhifa wa waziri mkuu.
Watu wengi walijitokeza siku ya uchaguzi, karibia asilimia 80, kulingana na makadirio ya awali ya tume ya uchaguzi.
Shughuli ya kuhesabu kura ilianza Jumatatu asubuhi, na matokeo ya mwisho bado hayajatolewa rasmi, lakini kiongozi wa upinzani Navin Ramgoolam alionekana kuchukuwa wadhifa wa waziri mkuu kwa mara ya tatu akiwa mkuu wa muungano wake wa Alliance of Change.