Sakata ya senti za timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Nigeria juu ya malipo na marupurupu imeendelea huku Shirika la kimataifa la kuwatetea wanasoka FIFPRO na Shirikisho la Soka Nigeria, NFF wakijibizana juu ya hatma ya malipo ya wanasoka hao.
Kulingana na FIFPRO kupitia taarifa iliyotoa kwa niaba ya wachezaji wa Nigeria, inasema kuwa wachezaji hao wa kike wa Super Falcons wanaamini kuwa ni wakati mwafaka wa Shirikisho la Soka la Nigeria NFF kutimiza ahadi zake na kukamilisha malipo kwa wachezaji.
"Inasikitisha kwamba wachezaji walihitaji kubishana na shirikisho lao wakati muhimu sana katika maisha yao ya soka." FIFPRO iliandika.
Timu imeghadhabishwa sana ya kwamba imelazimika kufuata Shirikisho la Soka la Nigeria kwa malipo yake kabla na wakati wa dimba na huenda ikalazimika kuendelea kufanya hivyo hata baada ya Kombe la Dunia.
Hata hivyo kwa upande wake, Shirikisho la soka la Nigeria linasema kuwa itatimiza ahadi ya kulipa pesa hizo mara tu itakazopokea malipo ya pesa za Kombe la Dunia na kama tu ilivyokuwa imewahakikishia wachezaji kabla ya Kombe la Dunia kwamba itawalipa mechi kadhaa za kirafiki na mechi za kufuzu ambazo walikuwa wakidai pamoja ada za kuonekana na bonasi mtawalia.
Ikakumbuka kuwa viongozi wa NFF walikaa na kukubaliana na wachezaji hao juu ya kiasi cha kuwalipa.
Aidha, Shirikisho hilo la Nigeria lilitoa pongezi timu hiyo kufuatia juhudi zake za kutinga hatua ya 16 bora na uhodari wake katika awamu ya makundi wa kutopoteza mechi moja kati ya nne ilizocheza kwenye muda wa kawaida na kusajili rekodi ya ajabu kwa timu ya Afrika.