Madeni ya ghafla yanaweza kukupeleka kwa watu wanaotoza riba ya juu kupita kiasi / Picha : Reuters 

Na Dayo Yusuf

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Kila inapofikia Januari, imekuwa kawaida kuona malalamiko mitandaoni, nyumbani na hata mitaani.

Misemo kama 'Januari ina siku themanini', au 'Januari mwezi wa kula kabichi na ugali,' na mengine mingi imejaa mitandaoni huku watu wakifanya mzaha na kucheka.

Lakini hili sio jambo la kucheka, inasikitisha hasa.

Uzito wa mwezi Januari umekuwepo miaka nenda miaka rudi na hauchagui wala haubagui. Lakini ni mwezi kama miezi mengine, kwanini uwe tofauti na miezi kumi na moja nyingine?

''Tatizo liko kwetu wenyewe kwa kukosa kujipanga,'' anasema Beatrice Kimaru, mtaalamu wa kiuchumi nchini Tanzania. ''Tunakuwa kama ndege. Hatupangi kwa ajili ya matukio yanayotukabili,'' anaongeza Beatrice.

Aghalabu Januari ndio mwezi ambapo wengi wanalipa ada, kodi za nyumba zinatakiwa, na vitu vingi vinakuwa vinanunuliwa upya au kubadilishwa.

''Watu wengi wanakuwa wameshatumia hela nyingi kutokana na shughuli nyingi zinazofanyika mwisho wa mwaka - Sherehe za Krismasi, ubarikio, kipaimara, ubatizo, na maharusi yote haya yanakusanyika kuanzia mwezi wa 9, 10 ,11 hadi 12,'' anaongeza Beatrice.

Umuhimu wa kujipanga

Lakini wataalamu wanaonya kuwa watu wengi hujisahau na majukumu yajayo baada ya Disemba na ndio maana Januari ikiingia inaonekana kuja na mzigo mzito.

Ukikosa kupanga matumizi ya fedha ulionayo mkononi utashindwa kupanga matumizi ya hela inayotarajiwa. / Picha : AA

''Januari inapaswa kupangiwa kuanzia Januari,'' anasema Beatrice. ''Suala la kulipa ada sio suala la emergency, kulipa kodi sio emergency. Unafahamu kwamba nina watoto ninawalea, wanapasa kwenda shule wanahitaji ada na madaftari. Anza kuweka akiba mapema kwa ajili ya matumizi haya yote. Kwa sababu hatupangi kwa ajili ya maisha yetu tunatumia hela bila kuweka mipango sahihi ndio maana inakua changa moto. Ndio unakutana na 'Njaa-nuari,'' anaelezea Beatrice.

Tatizo jengine linalowaathiri Waafrika wengi ni kujionyesha mbele za watu na hivyo wengi wanaishia kujiingiza katika gharama zisizo na umuhimu wowote.

Wataalamu wanasema tabia hii inawafanya wengi kulazimika kununua vitu vipya mfano wakati wa Krismasi au katika sherehe nyengine ilimradi watu waone mambo yamekaa sawa.

Kisaikolojia hili ni tatizo ambalo lisipodhibitiwa mapema linaweza kumwingiza mtu katika matatizo mengi zaidi ikiwemo kuingia katika mikopo isiyo na maana au hatimaye kushindwa kumudu, na hatimae kukubwa na sonona na msongo wa mawazo.

Madeni bila nidhamu

Ukikosa kupanga matumizi ya hela ulionayo mkononi utashindwa kupanga matumizi ya hela inayotarajiwa.

iwapo huna nidhamu ya kuweka akiba, basi afadhali uwe na desturi ya kuorodhesha matumizi kwa umuhimu zaidi. / Picha : TRT Afrika 

Ushauri huu umebainika hasa kwa wale wanaofanya matumizi ya hela ya ghafla. Ununuaji wa bidhaa ambazo hazikuwa kwenye bajeti unaweza kujikuta unatumia pesa kwa njia ambayo haikutarajiwa. Na hii hutokea mara nyingi wakati wa sikukuu na msimu wa mapumziko kama vile Disemba.

Ukosefu wa nidhamu ya matumizi pia inasababisha ukosefu wa nidhamu ya ukopaji.

''Wakati umejikuta na dharura ya pesa kwa kukosa kupanga matumizi yako vyema, kuna watu ambao wanatumia fursa hiyo kukukwamua,'' anasema Beatrice. '' Unakuta unalazimika kwenda kwa benki au Sacco au taasisi nyingine za fedha. Lakini hizi mara nyingi zinahitaji dhamana na kama huna basi unaishia kwa wale tunaowaita vibanda-umiza. Hizi ni kampuni au mtu binafsi ambaye anaweza kukutoza riba wakati mwingine nusu au hata zaidi ya nusu ya mkopo uliochukua. Usipojipanga kwa ajili ya maisha yako kuna watu watakupangia,'' anasema Beatrice.

Lakini Beatrice anashauri iwapo huna nidhamu ya kuweka akiba, basi afadhali uwe na desturi ya kuorodhesha matumizi kwa umuhimu zaidi.

''Hakuna aliyesema kuwa karo lazima zilipwe Januari. Iwapo unazo hela mkononi, basi timiza majukumu muhimu kama hayo ili hata na wewe unaweza kula krismasi ukijua karo ishalipwa,'' anasema Beatrice. '' Njia bora zaidi ni kusambaza malipo ndani ya mwaka mzima ili kuepusha malipo makubwa ya mara moja, yote kwa wakati mmoja,'' anaongeza.

Na kitu chengine ambacho kinawaumiza sana Waafrika wengi ni kushindwa kusema 'hapana.' Unatakiwa ujue kuwa sio kila kitu unaombwa au kuulizwa lazima ukubalie.

''Hasa msimu wa Krismasi au wakati wa Pasaka unakuta ndipo shughuli nyingi za kijamii zinawekwa hapo. Unakuta wewe mmoja una mchango wa harusi, ubatizo, na mambo mengine mengi. Na wakati mwengine hii michango unakuta imewekwa hela ya lazima ya kulipa. Ni lazima uwe unajipima uwezo wako umefikia wapi. Gharama za mwenzio za juu zisikuingize wewe katika gharama usizowezana nazo. Kumbuka kuna malipo yanakusubiri Januari,'' anasema Beatrice.

Gharama za mwenzio za juu zisikuingize wewe katika gharama usizowezana nazo. / Picha : TRT Afrika 

Desturi za kufuata

Wataalamu wa uchumi wanashauri kuwa kila kichohusu pesa katika maisha yako yanahusiana kwa namna moja au nyingine. Kwa hiyo ukivuruga sehemu moja utakuta unavuruga matumizi mengine.

Ili kuepuka madhara ya utumiaji mbaya wa fedha, kuna mambo muhimu ukifuata yatakusaidia kujiwekea nidhamu.

  • Usijiingize katika gharama ambazo hazina maana - mfano usinunue vitu kwa kutafuta sifa au kujionyesha kwa watu. Maoni ya watu hayakusaidii kumudu maisha yako.

  • Jitahidi kusambaza malipo katika mwaka mzima - Utajikuta unalipa hela kiasi kidogo kila mara kuliko kulipa kiasi kikubwa mara moja.

  • Panga matumizi yote katika bajeti ikiwemo hela za kujiburudisha - Hii itakusaidia kufuata nidhamu na kuepuka matumizi ya ghafla.

  • Usilazimishe vitu vya gharama ya juu - muhimu kabla ya kununua au kulipia kitu, uhakikishe kuwa ndicho cha bei bora zaidi, kwa kiwango hicho.

  • Sio lazima kukubali kila mualiko hasa inapogharimu pesa. Hata michango utoe kulingana na uwezo wako, iwapo lazima ushiriki.

  • Kengine cha muhimu ni kuweka kumbukumbu ya matumizi yako- itakusaidia kujua ni wapi ulipoteza pesa, ni wapi ulivuka bajeti na ni wapi utajiboresha katika mwaka mpya.

TRT Afrika