Na Mustafa Abdulkadir
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Waandamanaji wavamia Bunge kufuatia kupitishwa kwa muswada wa fedha 2024.
Vurugu kubwa zimeshuhudiwa ndani ya eneo la Bunge la Kitaifa la Kenya kufuatia kupitishwa kwa Muswada wa Fedha wa 2024.
Bunge hilo limepitisha muswada huo tata kwa kura 195 za NDIO na 106 zilizopinga muswada huo ambao umeibua maandamano kwa wiki ya pili mfululizo.
Kupitishwa kwa muswada huo kumeonekana kughadhabisha waandamanaji huku baadhi yao wakifanikiwa kuingia ndani ya majengo yenye ulinzi mkali nchini Kenya na kutaka kuondoka na Siwa ya Spika wa Bunge la nchi hiyo.
Huku hayo yakiendelea, baadhi ya waandamanaji walichoma sehemu ya jengo la Bunge huku wengine wakivamia na kuchoma moto sehemu ya la seneti.
Hapo awali, Rais William Ruto alisema kuwa vijana wana haki ya kuandamana na kuwa yuko tayari kukaa na vijana kujadili suala la muswada huo. Vilevile Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo, Kithure Kindiki, alitoa wito kwa waandamanaji alitoa wito kwa waandamanaji kuandamana kwa amani na bila kuharibu mali ya umma.
Hadi sasa watu wawili wanadaiwa kuuawa na polisi wakijaribu kuingia jengo la Bunge.
Kwa sasa, muswada huo unasubiria kusomwa kwa mara ya tatu kabla ya kupelekwa kwa Rais ambapo utaidhinishwa na kuwa sheria.
Maandamano hayo pia yameshuhudiwa katika miji mikubwa mengine nchini Kenya, kama Mombasa, Kisumu, Eldoret na Nakuru.
Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNHRC) imesema kuwa mtu mmoja ameuwawa wakati wa vurugu za kuingia ndani ya jengo la Bunge.