Masoko ya Jumapili yamekuwepo tangu 2021, jijini Addis Ababa, yakitoa soko mbadala kwa wananchi kupata vitu kwa bei nafuu . / Picha: AA

Wizara ya Biashara na Ushirikiano wa Kikanda nchini Ethiopia imetangaza kuanzishwa kwa viwango vya kuthibiti masoko ya Jumapili.

Masoko ya Jumapili yamekuwepo tangu 2021, jijini Addis Ababa, yakitoa fursa mbadala kwa wazalishaji, na wanaohitaji bidhaa tofauti kufanya biashara moja kwa moja bila madalali.

Biashara huwa ya bidhaa za kilimo na viwanda kwa bei nafuu.

Utawala wa jiji la Addis Ababa umepanua masoko haya ili kuhimiza miamala ya moja kwa moja kati ya wazalishaji na watumiaji, na zaidi ya maeneo 172 ya masoko ya Jumapili yanafanya kazi katika jiji lote.

"Masharti mapya pia yatajumuisha kanuni kuhusu wauzaji bidhaa, maeneo ya kuuza, vibanda, na bei," alisema Meskerem Bahiru, Mkurugenzi Mkuu wa Biashara ya Ndani katika Wizara ya Biashara na Ushirikiano wa Kikanda.

Viwango hivi vimetengenezwa ili kuhakikisha udhibiti, ufikiaji, na utoaji wa bidhaa na huduma bora kwa watumiaji katika masoko ya Jumapili.

Meskerem amesema viwango hivyo vitatumika hasa kwa aina sita ya bidhaa: mboga, matunda, mbegu za mafuta, nafaka, bidhaa za wanyama na bidhaa za viwandani.

Masoko ya Jumapili yamekuwa muhimu hasa huku gharama ya maisha nchini humo ikipanda kwa kasi tangu 2020.

Hii ni baada ya vita kati ya jeshi la taifa na kikundi cha TPLF cha kaskazini, ambavyo vilidumu kwa miaka miwili.

Vita hivyo viliathiri uzalishaji wa chakula katika maeneo yaliyokumbwa na vita na hapo kuathiri usambazaji wa bidhaa na hatimae madalali kuchukua fursa ya kudai zaidi.

Vikwazo vya kutoka Umoja wa Ulaya na Marekani kwa sababau ya vita hiyo pia vimeathiri uzalishaji nchini humo.

TRT Afrika