Na Coletta Wanjohi
Tarehe 5 Disemba 2022 viongozi wa kiraia na kijeshi wa Sudan walitia saini makubaliano ya kugawana madaraka ambayo yangefungua njia kwa mpangilio wa kikatiba ambao utasababisha nchi hiyo kufanya uchaguzi mwaka 2024.
Sudan imekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu 2021 wakati rais wa wakati huo Omar El Bashir alipopinduliwa na jeshi. Mgogoro kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Rapid Response Forces, nchini Sudan ambao ulianza tarehe 15 Aprili 2023, sasa unaongeza shinikizo kwa changamoto iliyopo katika bara, mabadiliko ya serikali kinyume na katiba.
Umoja wa Afrika, jumuia ya mataifa 55 ya Afrika inatambua utawala wa kiraia peke yake. Nchi nyingine tatu barani Afrika ziko chini ya utawala wa kijeshi kufuatia mabadiliko ya serikali kinyume na katiba.
Mnamo 2021 jeshi lilichukua mamlaka nchini Mali na Guinea na mnamo 2022 utawala wa kiraia wa Burkina Faso uliondolewa.
Desire Asogbavi mtaalam wa mahusiano ya kimataifa anasema serikali zinashindwa kukidhi mahitaji ya watu wake hasa vijana.
"Kutokuwa na uwezo wa kushughulikia mahitaji muhimu ya kijamii na kiuchumi ya idadi ya watu inayoendelea kukua na mahitaji ya vijana barani Afrika, hii ilikuwa kesi nchini Sudan na Mali na kwa kiasi fulani Guinea," Desire Asogbavi mkurugenzi wa Afrika wa Francophone, anaiambia TRT Afrika.
Mwaka wa 2022, majaribio ya mapinduzi ya serikali huko Guinea Bissau, Gambia na kisiwa cha Sao Tome na Principe yalishindwa.
"Mamlaka na taratibu zisizo za msingi ambazo zilianzishwa kipindi cha ukoloni na makampuni yao ya kimataifa zimekuwa zikitekelezwa katika ngazi za kisiasa na kiuchumi, kuchelewesha mchakato wa maendeleo katika maeneo ya Afrika, haikubaliki tena na vijana wa leo wenye ujuzi na uhusiano wa hali ya juu barani Afrika," Desire anaongeza. .
Mali, Guinea, Burkina Faso na Sudan zimesimamishwa kushiriki shughuli za Umoja wa Afrika kwa muda wote zitakao kuwa chini ya utawala wa kijeshi.
Katika mazungumzo ya amani na usalama Afrika afisa katika mpango wa mipaka wa umoja wa Afrika Fred Ngoga anasema muhimu ni serikali sikivu.
"Changamoto kubwa ya kizazi hiki ni kuunda serikali sikivu ambazo zinaweza kushughulikia mahitaji ya wananchi wao," Fred Ngoga Gateretse, afisa wa Umoja wa Afrika alielezea kwenye mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Mafunzo ya Usalama huko Addis Ababa, Ethiopia.
Nchi nne zilizo chini ya utawala wa kijeshi hazikuruhusiwa kushiriki katika mkutano wa marais wa Umoja wa Afrika wa kila mwaka ambao ulifanyika tarehe 18 na 19 Februari nchini Ethiopia.
"Tunafanya maamuzi ya kuweka vikwazo kwa nchi zilizo chini ya utawala wa kijeshi , pia tunaelewa kuwa vikwazo vya kiuchumi vinaathiri mfumo wa kijamii wa nchi hizo," Moussa Faki Mahammat mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika alisema wakati wa mkutano wa kilele wa AU.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, imeamua kuweka marufuku ya kusafiri kwa wanachama wa serikali na maafisa wengine wakuu kutoka Mali, Burkina Faso na Guinea.
"Tunaangalia vikwazo vilivyolengwa moa kwa moja hasa wale ambao ni wahusika wa mabadiliko hayo kinyume na katiba ya serikali ili watu wasiteseke," alisema Faki.
Baadhi ya vikwazo vikali ambavyo viliondolewa kutoka nchi za Afrika Magharibi ni pamoja na nchi jirani kufunga mipaka yao na nchi zilizoathiriwa na mapinduzi, kusitishwa kwa miamala ya kibiashara na miamala ya kifedha na kufungia mali ya nchi hizo katika benki kuu za kikanda na kibiashara za Afrika Magharibi.
Udhuru wa Uhuru
Mamlaka ya kujitawala huipa nchi huru haki ya kuitaka ishughulikie mambo yake ya ndani bila kuingiliwa na nje, kwa mfano kutoka kwa Umoja wa Afrika.
"Ukiangalia nchi ambazo zimesimamishwa kutoka Umoja wa Afrika, kusimamishwa kwao kunaonekana kuwa tuli sana,hatuoni hatua nyingi,” alisema Dkt. Andrews Atta-Asamoah, mkuu wa Programu ya Utawala wa Amani na Usalama ya Afrika katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama,
"Ni kama Umoja wa Afrika unajitahidi sana bila kufaulu kupata matokeoa yanayo hitajika kwa ajili ya kuwarejesha tena katika hali ya kawaida.”
"Tatizo linapokuja sio kwa sababu Umoja wa Afrika ulikuwa umeshindwa," balozi Churchill Monono mwakilishi wa Cameroon katika Umoja wa Afrika alielezea, kwani hata nchi yake Cameroon ni mwanachama wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.
“Tatizo linaonekana pale (AU) wanapowashauri wanachama kuwa wana tatizo, huwa wanasikiliza? Wanasema wako huru.
"Kuna wakati AU ilikuwa imepanga kwenda kujadili na baadhi ya serikali ambapo onyo la mapema lilikuwa limeonyesha kuwa wana matatizo, lakini serikali zilikataa,” alisema Monono.
Wanajeshi nchini Burkina Faso na Mali wameahidi kuwa na uchaguzi katika nchi zao mwaka 2024 ili kuwezesha mpito wa kidemokrasia wa mamlaka kwenda kwa utawala wa kiraia.