Rwanda imekusanya tani 2,280 za plastiki kwa ajili ya kuchakatwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Hii imewezekana kwa muungano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira ya Rwanda (REMA) na Shirikisho la Sekta Binafsi (PSF).
Ukusanyaji wa taka za plastiki chini ya ushirikiano wa REMA-PSF ulianza Mei, 2022, ukitekelezwa na kampuni mbili, 'Enviroserve Rwanda Green Park' na 'We Can Recycle'.
Kampuni ya 'We Can Recycle' ilichukua jukumu la ukusanyaji wa mifuko na chupa za plastiki baada ya mkataba wa kampuni ya 'Enviroserve' kumalizika, 'Enviroserve' likuwa tayari imekusanya zaidi ya tani 930, mwishoni mwa Septemba 2023," amesema Philbert Nkurunziza, Meneja wa Mpango wa Uokoaji na Udhibiti wa Uchafuzi wa Mazingira, (REMA).
"Kufikia Agosti 8, 'We Can Recycle' ilikuwa imekusanya tani 1,350 za mifuko na chupa za plastiki. Hivyo, jumla ya plastiki iliyokusanywa kuanzia Mei 2022 hadi Agosti 2024 ni tani 2,280,” Nkurunziza alifafanua.
Mwaka 2008, Rwanda ilikuwa mojawapo ya nchi za kwanza duniani kupiga marufuku mifuko na chupa ya plastiki.
Kampuni za kuchakata taka zinasema kuwa Rwanda inahitaji uwezo wa kukusanya zaidi ya tani 6,000 za taka za plastiki zinazotumika mara moja kila mwaka.
Taka za plastiki zinazokusanywa kwa matumizi moja hupondwa ili kuzalisha malighafi ya kuzalisha bidhaa nyingine, kama vile mapipa ya takataka,mitungi ya maji na vifaa vya kupakia bidhaa.
Mbali na uhifadhi wa mazingira, Rwanda inalenga kuongeza nafasi za ajira kwa miradi ya kuchakata plastiki.