Mwalimu

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Ni ukweli usiopingika kuwa lugha ya Kiswahili imefikia mamilioni ya wazungumzaji Afrika na ulimwenguni kwa ujumla.

Kati ya hao, yupo Shimaa Tarek, mzaliwa wa nchini Misri ambaye anashangaza watu kutokana na uhodari wake wa kuzungumza Kiswahili.

Tofauti na watu wengi, Shimaa, ambaye ana umri wa miaka 25, alianza kujifunza lugha adhimu ya Kiswahili akiwa na miaka nane tu.

Shimaa akiwa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri, Dkt. Emmanuel Nchimbi./Picha: Shimaa

“Nimezaliwa nchini Misri na nilianza kujifunza Kiswahili nikiwa binti mdogo tu,” anasema Shimaa katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Kulingana na Shimaa mwenyewe, alianza kusikia lugha hiyo ikizungumzwa Afrika Mashariki ndipo alivutiwa na kuamua kujifunza lugha hiyo.

“Nilivutiwa na lugha hiyo kwa sababu ya urahisi wake, hasa kutokana na kuwa ina maneno mengi kutoka lugha ya kiarabu, jambo hili lilinifanya niweze kuielewa kwa haraka,” anaelezea.

Shimaa akiwa kwenye moja ya mijadala ya Kiswahili./Picha: Shimaa

Shimaa anasema ilimchukua miaka minne kuanza kuzungumza kwa ufasaha lugha ya Kiswahili.

Kwa sasa, imekuwa ni jambo la kawaida sana kumuona Shimaa akizungumza lugha ya Kiswahili kwa ufasaha zaidi, hasa anapokuwa katikati ya wajuzi wa lugha hiyo.

Kama anavyosema mwenyewe, lugha ya Kiswahili imekuwa sehemu ya maisha yake hasa anapokuwa katikati ya wageni kutoka mataifa mbalimbali, japo hujawahi kutembelea nchi zinazozungumza lugha hiyo.

“Ni vyema uwe mwanafunzi mzuri na msikivu unapokuwa kwenye safari ya kujifunza lugha mpya, nadhani hiyo ndiyo siri kubwa kwangu ingawa sijawahi kutembelea nchi zenye kuzungumza lugha hiyo.

Kivutio mbele za watu

Uwezo wake wa kuzungumza lugha hiyo kwa ufasaha umemfanya Shimaa kuwa mfasiri wa lugha hiyo huku watu wengi wanayevutiwa naye wakitaka awe mkufunzi wa lugha hiyo pia.

Ukuaji wa Kiswahili nchini Misri

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limetambua mchango wa Shimaa katika kukuza Kiswahili./Picha: Shimaa

Shimaa anaamini kuwa lugha ya Kiswahili imeanza kuenea vizuri nchini Misri kuliko wakati mwingine wowote, huku watu wengi wakionesha nia ya dhati ya kujifunza lugha hiyo.

Kulingana na Shimaa, kwa sasa, lugha ya Kiswahili imeanzwa kufundishwa kwenye vyuo vikuu vinne nchini Misri, ambavyo ni Ain Shams, Al-Azhar, Cairo na Aswan.

Fursa zitokanazo na Kiswahili

Kama ilivyo kwa lugha zingine, Kiswahili ina fursa lukuki kwa wazungumzaji wake.

“Kwanza, wanaosoma lugha ya Kiswahili watapata faida ya kufahamu utamaduni wa Afrika Mashariki na historia yake na vile vile kuweza kutembelea eneo hilo ambalo nchi chimbuko la lugha hiyo,” Shimaa anasema.

Si hayo tu, wazungumzaji wa lugha hiyo pia wana fursa ya kupata ajira kupitia kwa lugha ya Kiswahili, kama ilivyo kwa Shimaa mwenyewe, ambaye kwa sasa ni mhadhiri wa lugha ya Kiswahili nchini Misri.

TRT Afrika