Kituo cha Maendeleo ya Sheria (Law Development Center, LDC ) kinataka Baraza la Sheria la Uganda kuchunguza uwezekano wa ongezeko ya shahada bandia kutoka vyuo vikuu vya Uganda/ Picha: AFP

Kituo cha Maendeleo ya Sheria Uganda (Law Development Center, LDC ) kinataka Baraza la Sheria la Uganda, chombo kilichopewa mamlaka ya kudhibiti taaluma ya sheria nchini humo, kuchunguza uwezekano wa ongezeko ya shahada bandia kutoka kwa baadhi ya vyuo vikuu nchini humo.

LDC ni taasisi ya elimu nchini Uganda inayotoa masomo ya juu mbalimbali ya kisheria na huchukua wanafunzi waliomaliza shahada ya sheria katika vyuo vikuu, ili waongeze masomo kwa muda wa mwaka mmoja kabla ya kuingia katika soko ya sekta ya sheria.

Annet Karungi afisa mkuu kutoka Chuo cha LDC alikuwa mbele ya kamati ya sheria ya bunge, akisema kuwa kumekuwa na ongezeko ya shahada nyingi za vyuo vyuo vikuu, jambo ambalo si la kawaida.

Wabunge wameitaka LDC kueleza ni kwa nini baadhi ya wanafunzi hawakupokelewa katika kituo hicho, licha ya kulipia kozi hiyo.

"Unapata Waafriaka kutoka vyuo vikuu vyengine, takriban darasa mzima kama 600 wote wako na shahada ya daraja la kwanza au la pili, kwa hivyo ilibidi tutumie mbinu tofauti, na tukaamua kuchukua asili mia 60 tu ya waliomba nafasi," Karungi alielezea,

Wabunge walimuuliza Karungi iwapo wale wanafunzi wanakuja na shahada ya juu zaidi wanaonyesha kuwa kweli uelewa wao wa masomo ni wa kiwango cha juu.

"Tukiangalia mtindo katika miaka michache iliyopita wanafunzi ambao wanakuja na shahada za juu sio wanafunzi wa ubora sana baadaye wanapojiunga na sisi, na wengi wao wanapatikana wakirudia rudia masomo na hapo kuzuia wengine kupata nafasi pia," ameongezea.

"Kwa hiyo, ni jambo ambalo tumeliambia Baraza la Sheria na tunatumai kama mdhibiti, watalisimamia na kulishughulikia wakati wa udhibiti na uidhinishaji wa sheria za shule au vyuo vikuu," Karungi alisema.

Suala hili la shahada bandia linakuja huku serikali ya Nigeria pia ikitangaza ongezeko ya shahada bandia, Wizara ya Elimu ya Nigeria ilisema wiki iliyopita kuwa itasimamisha uidhinishaji wa digrii, ikijumuisha nchi kama vile Kenya na Uganda.

Uamuzi huu unafuatia kusimamishwa kwa hivi majuzi kwa uidhinishaji wa digrii zilizopatikana kutoka nchini Benin na Togo kwani zilibainika kuwa ni za bandia.

TRT Afrika