Muswada wa Sheria ya Taifa ya Walimu wa mwaka 2024 unapendekeza walimu wote wawe na shahada ya kwanza kabla ya kuajiriwa/ picha kutoka Wizara ya Elimu na Michezo Uganda 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Uganda Kiwanuka Kiryowa ametetea hitaji la walimu wote nchini humo kuwa na shahada ya kwanza kama hitaji la msingi kupata ajira.

"Nadhani kwa tathmini ambayo imetolewa na kufanywa na Serikali, hatukosi watu wenye kiwango hiki cha elimu. Sheria hii ilipotungwa tulikuwa hatuna haja walimu kuwa na shahada, sasa tunayo," Kiryowa ameiambia Kamati ya Bunge.

Alikuwa akijibu hoja zilizotolewa na wadau mbalimbali kuhusu Muswada wa Sheria ya Taifa ya Walimu ya mwaka 2024.

Irene Linda Mugisha mbunge wa wanawake wa mji wa Fort Portal alishangaa kwa nini Serikali ambayo haijawekeza au kumiliki shule za awali,au chekechea baada ya kuiachia sekta binafsi inadai walimu wa shule za chekekea wawe na shahada ya kwanza kama kiwango cha chini.

“Tunaweka kiwango cha Shahada ya Kwanza, hivi hizi taasisi binafsi zitalipa kiasi gani cha fedha? Hii ina maana kwamba, tunakwenda kuhamisha gharama kwa wazazi kwa sababu kama serikali, kwanza tumeshindwa kuwalipa walimu wetu," Mugisha alisema.

"Ukiangalia shule za msingi tumeshindwa kuwalipa walimu wote, hadi sasa wazazi wanalipa walimu kwa hiyo sasa tunasema hata kwa shule ya awali wawe na shahada ya kwanza na bado Serikali tumeshindwa kumiliki shule hizo. Shule hizi za awali, zinamilikiwa na taasisi binafsi. Kwa hivyo, hufikirii kwamba tunaenda kwa bidii kidogo?" Mugisha alimuuliza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mugisha alishangaa ni kwa nini Serikali haizingatii fursa ya kuanzisha malipo ya kitaaluma ili kuwapa motisha walimu hao ili wapandishe sifa zao za elimu. Kwa mfano, kuhakikisha kuwa mwalimu akipata shahada ya kwanza, atalipwa moja kwa moja zaidi ili kuwawezesha walimu hao kupandisha madaraja yao taratibu badala ya kuwalazimisha.

Lakini Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisisitiza kuwa uamuzi wa serikali unawakilisha matarajio ya wananchi.

“Sheria hizi zinazungumzia matarajio ya watu wa Uganda, tunatamani kuona nini? Na tunachotamani kuona ni mfumo wa elimu ambao kwa hakika ni mahiri na unaojali mahitaji ya wanafunzi na pia walimu. Lakini matarajio yetu ni kuwa na watu wa elimu ya awali wanaosomeshwa na watu wenye shahada na sifa zinazohitajika kama zitakavyowekwa mara kwa mara na Baraza kwa kushauriana na Serikali,” alifafanua Kiryowa.

Amesema watu ambao wako serikalini sasa, lazima wafanye kazi ya kubadilisha mfumo wa mahitaji ya walimu. Wamepewa muda wa miaka 10 wa mpito wa kutimiza haya.

Amesema ikiwa hawatabadilika kwa miaka 10 na sheria ikabaki kama ilivyo, wataondolewa kwa sababu watu walio na shahada ya kwanza wataingia katika soko la ajira.

TRT Afrika