Idadi ya vifo nchini Sudan kutokana na mlipuko wa kipindupindu imeongezeka hadi 315, huku waliofariki kutokana na mafuriko na mvua kubwa ikifikia 225, mamlaka ya afya ya nchi hiyo ilisema Jumatatu.
Wizara ya Afya ilisema katika taarifa yake kwamba visa vipya 266 vya kipindupindu vilisajiliwa, na kufikisha jumla ya 9,533 ya maambukizi tangu Agosti na vifo 315.
Mamlaka ilitangaza kipindupindu kuwa janga nchini Agosti 12.
Katika ripoti hiyo hiyo, wizara hiyo ilisema idadi ya vifo kutokana na mafuriko na mvua kote Sudan imefikia 225, huku wengine 889 wakijeruhiwa.
Zaidi ya nyumba 35,794 zimeharibiwa vibaya, huku 40,781 zimeharibiwa kwa kiasi kutokana na mvua hiyo iliyoanza tangu Juni, iliongeza.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilitangaza kuwa zaidi ya Wasudan 178,000 wamekimbia makazi yao kutokana na mafuriko na mvua katika majimbo 15 kati ya 18 tangu Juni mwaka huu.