Serikali ya Kenya imesema imeweka hatua madhubuti kukabiliana na athari za mvua za El Nino ambazo zinatarajiwa kuanza katikati ya mwezi Oktoba na kuendelea mpaka mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu.
Katika mkutano na wadau mbalimbali, ambao mwenyekiti wake alikuwa Naibu Rais wa nchi hiyo Rigathi Gachagua, amesema serikali inakadiria kwamba inahitaji kiasi cha shilingi bilioni 10 za Kenya ambazo ni sawa na dola milioni 67 ili kukabiliana na athari za El Nino hasa katika maeneo ya ukame.
Mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha mwaka huu, wataalamu wanasema zitakuwa na athari kubwa zaidi kuliko zile za mwaka 1997.
“Tunaona katika makadirio yetu, tutahitaji shilingi za kenya bilioni 9.3 kwa maeneo yenye ukame,” amesema Waziri wa Afrika Mashariki wa Maendeleo ya Maeneo yenye Ukame, Rebecca Miano.
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Ann Waiguru ameongeza: “Kaunti nne, tumekisia kutenga shilingi bilioni 15 za Kenya kusaidia kusambaza chakula kwa watakaohama makazi yao.”
Naibu Rais Gachagua, hata hivyo, aliyatahadharisha mashirika yaliyohudhuria mkutano, kutotumia fursa ya janga la El Nino kujinufaisha kwa kutumia vibaya fedha ya walipa kodi.
“Pia ni muhimu kujua kwamba nchi yetu haiko vizuri kiuchumi...tuwe na busara katika mipango yetu wa fedha, tusikuze mambo,” alisema.
Wakati huo huo, serikali pia imetabiri kwamba, mvua za El Nino zitaathiri tarehe za mitihani ambayo imepangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba.
“Pia ni muhimu kujua kwamba nchi yetu haiko vizuri kiuchumi...tuwe na busara katika mipango yetu wa fedha, tusikuze mambo.”
Waziri wa Ulinzi Aden Duale amewaambia washiriki wa mkutano huo kwamba tayari ameliweka jeshi katika hali ya tahadhari na vikosi vya anga vitasaidia kusambaza mitihani ya taifa katika maeneo ambayo yatakuwa yameathiriwa vibaya kutokana na mvua hizo.
“Tunajua barabara nyingi zitakuwa zimeharibika…tumeandaa helikopta zetu za jeshi kusaidia kupeleka mitihani katika vituo husika,” amesema Duale. Gachagua ameongeza kusema: “Lazima tujue kwamba kazi yetu kama serikali ni kuhakikisha hakuna Mkenya atakae kufa kutokana na mvua za El Nino, na kushindwa kupanga ndio kupanga kushindwa.”
Wakati huo huo, pia wito ulitolewa wa kuanza kusafisha mitaro huku wakionyesha wasi wasi wa madhara ya kiafya.
Baraza la magavana linaitaka KEMSA kusambaza dawa katika vituo vya afya kabla ya kuanza kwa mvua za El Nino.
“Tunawataka KEMSA waende kwa kasi inayotakiwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo, muhimu tupate dawa katika hospitali zote...El Nino italeta mlipuko wa magonjwa,” Mwenyekiti wa Baraza la Magavana la Afya Muthomi Njuki amesema.
Nae Waziri wa Fedha Prof. Njuguna Ndung’u ametakiwa kutoa taarifa kwa kamati ya kiufundi Jumanne wiki ijayo ili kuainisha rasilimali zilizopo ambazo zitatumika kipindi hicho cha El Nino.