Kaya 400 mashariki mwa Kenya zatakiwa kuhama makazi kuepuka athari za El Nino

Kaya 400 mashariki mwa Kenya zatakiwa kuhama makazi kuepuka athari za El Nino

Serikali na taasisi binafsi zinatakiwa kuwekeza rasilimali ili kusaidia familia kuhama maeneo ambayo ni hatarishi.
Kwa mujibu wa serikali ya Kenya, maeneo yatakayoathirika zaidi ni yale yaliyo chini ikiwemo mabonde.

Wananchi wanaoishi maeneo ya bonde katika kaunty ya Isiolo nchini Kenya wameshauriwa kuondoka katika maeneo hayo ili kuepuka hasara itakayosababishwa na mafuriko yatakayosababishwa na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha wakati wowote kuanzia sasa.

Tahadhari hiyo imetolewa huku serikali ya nchi hiyo ikiwa na wasiwasi kwamba, zaidi ya kaya 400 hasa kutoka maeneo ya Iresaboru, Garbatulla ambayo yanafahamika kwa mafuriko ya mto Ewaro Nyiro, wataathirika. Hata hivyo, taarifa zinaonyesha wakazi hao wanaonekana kusita kuhamia maeneo ambayo yametajwa kuwa salama zaidi katika kaunti hiyo.

Wakati huo huo, Duncan Kipkoech ambae ni msaidizi kamishna wa kaunti ya Garbatulla ameitaka serikali na taasisi binafsi kuwekeza rasilimali ili kusaidia familia kuhama maeneo ambayo ni hatarishi.

Sehemu kame ziko hatarini zaidi kukumbwa na athari ya mvua za El Nino kutokana na hali yake ya kijiografia na athari za ukame wa hivi karibuni

“Msisubiri mpaka mpaka mvua zilete madhara kwenu,” amesema bwana Kipkoech wakati wa usambazaji wa misaada isiyo ya chakula kwa kaya 100 zilizohama kutoka eneo la Iresaboru.

Nae Naibu Gavana James Lowasa ameitaka serikali kusaidia kaunti hiyo katika masuala ya uratibu wa chakula ili kuepusha maafa na uharibifu wa mali hasa katika maeneo ya Merti, Merti, Gafarsa na Sericho.

“Tumeanza kufanya maandalizi ya kukabiliana na El Nino, lakini tunahitaji kuungwa mkono na serikali kuu kwa sababu tumetoka katika ukame mbaya katika kipindi cha miaka 40 ambao umekuwa na athari kubwa kwa jamii,” amenukuliwa bwana Lowasa na baadhi ya vyombo vya habari nchini humo.

Ikumbukwe kwamba, katika mkutano wake wa hivi karibuni wa kujadili maandalizi ya mvua za El Nino na athari zake, Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua amesema kikosi cha NYS kitapelekwa kusaidia kukabiliana na madhara ya mafuriko.

Sehemu kame ndio ziko katika hali hatarishi pindi mvua hizo za El Nino zitakapoanza kutokana na hali yake ya kijiografia na athari ya ukame za hivi karibuni baada ya maeneo hayo kukosa mvua kwa kipindi kirefu hivyo kupunguza mazao na kuuwa idadi kubwa ya mifugo.

Baadhi ya maeneo ambayo yanatabiriwa kupata athari kubwa ya El Nino nchini Kenya ni pamoja na Garissa, Isiolo, Kilifi, Kwale, Marsabit, Narok, Tana River, Samburu, Taita-Taveta, Turkana na Wajir.

Mamlaka za Hali ya Hewa kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki tayari zimetabiri kuwepo kwa mvua hizo zinazotarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa na kuendelea hadi mwezi Disemba mwaka huu. Tayari tahadhari imetolewa kwa wale wanaokaa maeneo hatarishi ikiwemo mabondeni kuchukua hatua kabla ya mafuriko kutokea.

TRT Afrika