Mojawapo ya makaburi ya halaiki yaliyofukuliwa katika msitu wa Shakahola, pwani ya Kenya. Picha: Vyombo Mbalimbali

Mhubiri tata Paul Mackenzie na washtakiwa wengine wataendelea kushikiliwa kwa siku 47, Jaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Shanzu, Yusuf Shikanda ameamua.

Uamuzi wa mahakama unajiri kufuatia ombi la Serikali ya Kenya kupitia Mwendesha Mashtaka Mkuu wake Jami Yamina, wa kusaka muda zaidi ili kukamilisha uchunguzi wake.

Awali, Mackenzie na wenzake waliomba kuachiliwa kwa dhamana kwa Mackenzie baada ya kuwa gerezani kwa zaidi ya siku 90.

Mackenzie na wenzake watazuiliwa kwa siku hizo 47 kuanzia tarehe ya nyuma ya 2 Agosti, huku wakitishia kushiriki mgomo wa kutokula.

Aidha, wakili wa Mackenzie, Wycliff Makasembo, alipinga ombi hilo, huku akisema kuwa Upande wa Mashtaka ulishindwa kuwashtaki wateja.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wake Jami Yamina, aliomba muda zaidi wakiendelea kukusanya ushahidi kabla ya kufungua rasmi mashtaka ya jinai dhidi ya washukiwa hao.

Mwanzilishi huyo wa Kanisa la Good News International amekuwa akizuiliwa tangu mwezi Aprili baada ya kujisalimisha kufuatia ufichuzi wa makaburi ya halaiki yaliyofukuliwa katika msitu wa Shakahola, pwani ya Kenya.

TRT Afrika