Shirika la msalaba mwekundu nchini Kenya limesema kuwa limewaokoa wanafunzi 35 katika walichotaja kuwa 'ajali ya boti' Jumapili usiku.
Shirika hilo lilitangaza katika mtandao wake wa X kuwa wanafunzi hao ni miongoni mwa abiria 40 waliokuwa katika boti hilo lililokuwa likipita eneo lijulikanalo kama Ndia ya Ndovu, karibu na bandari ya Lamu.
Wakaazi waliozungumza na TRT Afrika wamesema kuwa abiria hao 'walikwama baharini', baada ya nahodha kuchukua mkondo usio sawa wakati maji ya bahari yalikuwa yameshuka na ndipo boti likagonga matumbawe na kutua juu yake.
''Wanafunzi hao walipiga simu waje waokolewe.'' mmoja wa wakaazi ameambia TRT Afrika. '' Kama sivyo wangelazimika kusubiri hata saa nane kabla maji kurudi sawa waweze kuendelea na safari.'' aliongeza.
Vifo vya baharini ni nadra katika eneo la Pwani ya Kenya, japo ajali hutokea mara kwa mara, zaidi kutokana na hali mbovu ya boti au mawimbi makali.