Katika makubaliano ya kupeleka maelfu ya wafanyakazi wa Kenya kutafuta ajira Saudi Arabia, wizara ya kazi na uhifadhi wa jamii imetangaza kuwa wauguzi zaidi watapewa fursa ya kuhamia nchi hiyo ya kiarabu.
"Serikali ya Kenya inashirikiana na Ufalme wa Saudi Arabia (KSA) katika kuimarisha uhamiaji salama, wa kawaida na wenye tija kati ya nchi hizo mbili," Wizara ya Kazi ilichapisha katika mtandao wake wa Twitter.
Wafanyakazi hao wa afya wanahitajika katika nyanja za uuguzi na matibabu, upasuaji, kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU), kitengo cha wagonjwa mahututi kwa watoto (PICU), na ukunga.
Fungu la mishahara ya wauguzi Saudi Arabia
- Mshahara - $1250
- Saa za kazi - 48 kwa wiki
- Tikiti ya ndege kurudi nyumbani kwa mwaka
- Makazi
- Bima ya Afya
- Usafiri, sare za kazi na marupurupu ya kazi ya ziada, miongoni mwa mengine.
''Waombaji watahitajika kutimiza mahitaji kama vile shahada ya chuo katika Sayansi ya Uuguzi au ukunga, uzoefu usiopungua miaka miwili katika uwanja huo, na cheti halali cha kibali cha polisi, kati ya zingine.'' Taarifa hiyo iliendelea kusema.
Hata hivyo kumekuwa na wasiwasi miongoni mwa Wakenya katika miaka ya hivi karibuni kutokana na ripoti za udhalilishaji wa wafanyakazi katika nchi za kiarabu.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesisitiza kuwa serikali inatakiwa kudhibiti upelekaji wa wafanyakazi hasa wale wasaidizi wa nyumbani katika nchi za kiarabu ili kupunguza unyanyasaji wao ambvao wakati mwingine huishia kwa kifo.
Mapema mwaka huu, mwenyekiti wa Muungano wa mauguzi na wahudumu wa afya KUCO Peterson Wachira, alisema kuwa sekta ya afya inatishiwa na janga iwapo serikali haitawaajiri wahudumu zaidi.
"Tuna madaktari wapatao 4,000 wasio na ajira ambao wamepatiwa mafunzo, maafisa wa kliniki 9,000 ambao hawana kazi, tuna wauguzi wapatao 20,000 ambao hawana ajira." Alisema Wachira.
Hata hivo Wizara ya kazi imesisitiza katika taarifa yake kuwa mikakati imewekwa kati ya Kenya na Saudi Arabia kuhakikisha mfumo wazi na wa haki unatumika katika kuwaajiri wauguzi hao.