Gift Dumedah
TRT Afrika, Ghana
Mwaka mpya umefika na bila shaka, malengo ya wana Afrika yanabaki kuwa yaleyale; kutafuta suluhu ya majanga yatokanayo na ajali za barabarani.
Kwa hakika, bara la Afrika limejiwekea malengo mahususi, ya kumaliza ajali barabarani zinazosababisha watumiaji kupata majeraha na hatimaye kupoteza maisha.
Kimsingi, bara la Afrika limeweka malengo la kuhakikisha usawa na usalama katika huduma za usafiri kwa watu wake.
Iwapo Afrika imenuwia kuukuza mkakati huu, itajihakikishia kuokoa maisha ya watu 27 kwa kila watu 100,000; na takriban asilimia 7 ya Pato la Taifa la kila mwaka (GDP) kwa nchi nyingi barani.
Hata hivyo, makisio haya hayajumuishi madhara ya kisaikolojia kwa waathirika wa ajali za barabarani.
Takribani watu 3,609 walipoteza maisha kwa ajali za barabarani nchini Kenya. Vifo hivyo viliripotiwa kati ya mwezi Januari na Oktoba mwaka jana.
Vivyo hivyo, watu 1,839 waliangamia barabarani na wengine 12,678 kujeruhiwa nchini Ghana.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), nchi za Nigeria, Ethiopia, Afrika Kusini na Sudan zikiongoza kwa jinamizi la ajali za barabarani, kusini mwa jangwa la Sahara.
Kadhalika, nchi ya Nigeria ndio kinara wa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani.
Nchi hiyo, ambayo ni ya tatu kwa uzalishaji wa mafuta barani Afrika, ina kiwango cha juu cha vifo 52.4 kati ya 100,000 kwa kila nchi duniani. Msumbiji inafuata kwa karibu vifo 46.7 kati ya watu 100,000 duniani.
Jukumu la pamoja
Ni ukweli usiopingika kuwa jukumu la kupunguza jinamizi kwenye barabara nyingi linawezekana kwa sababu ajali za barabarani zinaepukika. Ukweli huu unakuja wakati WHO inaripoti kuwa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani, kati ya 2010 na 2021 vinapungua, isipokuwa kwa bara la Afrika ambalo limeshuhudia asilimia 17 tu ya upungufu huo, ilhali idadi ya vyombo vya moto na miundombinu ya barabara bado chache na duni, ikilinganisha na mabara mengine.
Ni ukweli usiopingika kuwa, kutokana na hali ya uchumi barani Afrika, wananchi wengi huagiza vyombo vya moto kutoka ng’ambo na asilimia kubwa ya magari hayo hayakidhi vigezo vya matumizi ya barabarani.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani inaeleza bayana kuwa hatua kubwa inapigwa katika nchi zilizoamua kupitisha mifumo salama ya matumizi ya barabara.
Mifumo hiyo imeweka msisitizo kuwa usalama ni wajibu wa kila mmoja wetu; kutoka kwa watumiaji wa barabara, wasimamizi wa barabara, wabunifu, wajenzi, watunzaji wa mfumo wa barabara na watoa huduma baada ya ajali.
Mfumo huo unaongozwa na misingi mikuu mitano ambayo inasisitiza kuwa: vifo na majeruhi wa barabarani havikubaliki, watu hufanya makosa barabarani, watumiaji wa barabaraba huwa kwenye mazingira hatarishi ya ajali, kuwa ni vyema kuchukua hatua ili kupunguza ajali vyengine na umuhimu wa kutoa suluhisho kwa viashiria vipya vya ajali.
Kwa kuzingatia kanuni na vipengele hivi, mbinu ya mfumo salama inalenga kuunda mazingira salama ya barabarani na kupunguza idadi ya ajali za barabarani, vifo na majeruhi.
Namna ya kusamehe makosa
Kando na mtazamo wake unaolenga matokeo, mfumo salama ni mbinu pana yenye vipengele vya kipekee.
Inalenga binadamu, ikizingatia usalama wa watumiaji wa barabara kwa kufanya mabadiliko kwa matumizi ya vyombo vya moto na muundo wa barabara huku ikishughulikia na kuzingatia kasoro za kibinaadamu.
Mbinu hii pia, inabeba mtazamo wa mfumo mzima kwa kushughulikia mifumo, sera, na mazingira halisi, ikiwa ni pamoja na muundo wa barabara, muundo wa gari na usimamizi wa kasi.
Mbinu hiyo hutumia muundo wa kusamehe makosa kwa kusisitiza kuwa mfumo wa usafirishaji unapaswa kuundwa na kuendeshwa ili kupunguza madhara, huku ikikubali kuwa watumiaji wa barabara hufanya makosa na wakati mwingine maamuzi mabaya.
Na pia kwamba, mwili wa binadamu una kikomo cha kuvumilia ajali za barabarani kabla ya vifo au majeraha makubwa.
Hatari zaidi kuliko magonjwa
Mbinu ya mfumo salama hutumika kushughulikia masuala ya usalama yanayohusiana na miundombinu, tabia ya binadamu, uangalizi unaowajibika wa sekta ya magari na uchukuzi, na majibu ya dharura.
Pamoja na matokeo chanya ya mfumo huo, bado nchi nyingi za Kiafrika zinashindwa kuutekeleza.
Kimsingi, kuna masuala mtambuka na changamoto kadhaa zinazofanya nchi nyingi Afrika kushindwa kuupitisha mfumo huu, kama sio kuufanya sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Sababu kuu kati ya nyingi ni kuwa suala la usalama barabarani halijapewa kipaumbele katika nchi nyingi za Kiafrika, na bado halionekani kama ni tatizo.
Hii inadhihirishwa na rasilimali finyu zinazotengwa katika kukuza usalama barabarani na kupunguza majeraha.
Kwa mfano, mpango mkakati wa usalama barabarani Afrika unazitaka nchi za Afrika kutenga angalau asilimia 10 ya uwekezaji kwenye miundombinu ya barabara kwenye usalama barabarani.
Ingawa ni vigumu kuthibitisha mgawanyo halisi wa kitaifa, bado kuna changamoto zinazohusiana na rasilimali chache, vipaumbele vinavyoshindana, na dhamira ya kisiasa.
Kulingana na WHO, majeraha yatokanayo na ajali za barabarani ndiyo sababu kuu ya vifo baada ya Malaria na Kifua Kikuu.
Hata hivyo, bado haipewei msukumo unaostahili katika uwekezaji haswa wa rasilimali fedha, miundombinu ifaayo na tafiti.
Kinachokosekana
Hata hivyo, kuna fursa si haba kwa mwaka 2024 za kufanya maendeleo ya kweli kuhusu kukuza usalama na kuzuia majeraha kupitia mbinu ya mfumo salama barani Afrika.
Idadi kubwa ya miundombinu ya usafiri na uhamaji bado inajengwa barani Afrika, kwa matarajio ya kuunganisha viwango vya usalama moja kwa moja.
Hata hivyo, hili halitotegemea maajabu bila jitihada madhubuti na za kimakusudi.
Usalama wa maisha ya binadamu lazima upewe kipaumbele kwenye barabara zetu.
Ahadi ya kuwa na maono sifuri katika kuokoa maisha kwenye barabara zetu inaweza kufikiwa kupitia mbinu ya mfumo salama. Hata hivyo, kipengele kinachokosekana ni hatua za dhati kwa pande zote, yaani watumiaji wa barabara, watunga sera, wabunifu, wajenzi, watunzaji wa mfumo wa barabara na watoa huduma za baada ya ajali.
Ni matumainio ya kila muafrika wa kuwa na mfumo salama wa usafiri usio na vifo na majeraha yanayohudumia watumiaji wote wa barabara.
Mwandishi wa Makala hii ni msomi kutoka Ghana ambaye andiko tafiti yake imeangazia uhakika wa huduma za usafiri Afrika.